Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kukamilisha ujenzi taasisi ya sayansi za bahari zanzibar

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya majengo ambayo
hayajakamilika na ķusikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya
Sayansi za Bahari Dkt. Magreth Kyewalyanga alipotembelea Taasisi hiyo
kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali.

Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akitoa maelekezo kuhusu namna ya
ukamilishaji wa miundombinu ambayo haijakamilika kwa Mkurugenzi wa
Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu, Zanzibar Dkt. Magreth Kyewalyanga
alipotembelea Taasisi hiyo.

Mbunge wa Kiembe Samaki Mhe.
Mohammed Maulid akizungumza katika kikao cha waziri na watumishi wa
Taasisi ya Sayansi za Bahari, wakati Waziri alipofanya ziara katika
Taasisi hiyo Buyu, Zanzibar

Muonekano wa moja ya majengo ya Taasisi ya Sayansi za Bahari yaliyopo Buyuni Zanzibar yaliyokamilika kujengwa

…………………………………………………………………

Serikali kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imeahidi kukamilisha ujenzi wa majengo katika
Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo
Buyu, Zanzibar

Akizungumza baada ya kukagua chuo
hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
amesema Wizara kupitia mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu tayari
imeshatenga zaidi ya Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa
mabweni katika Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako amesema mbali ya
fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona
namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo ambayo tayari
misingi yake imeshajengwa na imekaa muda mrefu bila kukamilishwa.

“Mbali ya kutenga fedha za ujenzi
wa mabweni, lakini mimi na Katibu Mkuu tulishaanza kufanya mapitio
miradi tuliyonayo katika wizara kuona inawezaje kusaidia kukamilisha
ujenzi wa majengo yote yaliyoishia katika hatua ya msingi ambayo ni
muhimu katika kukamilisha mafunzo,” amesema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo amesema kamwe Serikali
haiwezi kuona fedha zilizotumika kujenga misingi hiyo zinapotea bure
kwa kuwa hakuna fedha za kukamilisha ujenzi. Amesema matamanio yake ni
kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika
mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe
ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.

Aidha, ameupongeza uongozi wa
Taasisi hiyo kwa kuanza masomo pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali,
amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan juu ya kuandaa vijana
wenye ujuzi ambapo Taassisi hiyo ina Programu za mafunzo mbalimbali
ambayo yanatoa ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.

Naye Mbunge wa Kiembe Samaki
ambapo Taasisi hiyo ipo Mhe. Mohammed Maulid amemshukuru Waziri kwa
kufika katika Taasisi hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa taifa katika
kuandaa wataalamu wa sayansi ya majini ambao wataiwezesha kufanikisha
uchumi wa bluu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Taasisi ya Sayansi za Bahari Dkt.Magreth Kyewalyanga amemwambia waziri
kuwa ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyo kwenye hatua ya msingi
zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni saba na milioni mia tano.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa
Serikali ya wanafunzi DARUSO Frank Buluma amesema Taasisi hiyo
imewasaidia wao kama vijana kupata fursa ya kupata elimu ya Sayansi
ambayo itawawezesha kushiriki katika kukuza uchumi kupitia uchumi wa
bluu. Ametoa wito kwa vijana kujiunga na chuo hicho ambacho
kitawawezesha kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri katika eneo jipya
la ajira.

Taasisi ya Sayansi za Bahari,
inatoa mafunzo katika ngazi umahiri, uzamivu na shahada za awali,
kufanya tafiti na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ya Sayansi ya
Bahari.