Katibu Tawala Msaidizi Uchumi Bw.
Ellias Luvanda (kulia) akikabidhi tuzo ya kutambua utendaji mzuri katika
uagizaji wa Mbolea kwa pamoja iliyotolewa na Mamlaka ya Mbolea TFRA ,
akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Iringa (IFCU) Bw.
Victor Mwipopo (kushoto) wakati wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho
mkoani Iringa
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akieleza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho mkoani Iringa
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama Kikuu cha Ushirika IFCU Wakifuatilia taarifa wakati mkutano huo ukiendelea
Viongozi wa Vyama vya Ushirika
wamepewa wito kusimamia matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili
kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao yao na bei zenye tija kwa
kuweka vipaumbele vya mipango ya ujenzi wa maghala kuanzia ngazi ya
vijiji.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa
Mkoa wa Iringa kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu
tawala Msaidizi Uchumi Elias Luvanda wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 20
wa mwaka wa wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa IFCU
(1993) Ltd, uliofanyika Ijumaa Mei 07, 2021 Mkoani Iringa.
Katibu Tawala Msaidizi Luvanda amesema
Serikali inahamasisha na kuendeleza wakulima kwa kuhakikisha Mfumo wa
Stakabadhi ya Ghalani unaimarika.
Hivyo, amewataka Viongozi katika mkutano
huo kuweka mipango yenye malengo ya kuongeza maghala ya kuhifadhi mazao
ya wakulima ili kukabiliana na changamoto ya uchache wa maghala na
kuzingatia matumizi bora ya maghala.
Aidha, amewataka viongozi wa Ushirika
kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali za Vyama vya Ushirika, kuwajibika
kwa wanachama wao kwa kufuata misingi na taratibu za Ushirika
zitakazosaidia kuondokana na matumizi mabaya ya mali iza vyama pamoja na
ubadhilifu.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt.
Benson Ndiege akiongea kwa niaba ya wanaushirika amesema Vyama vya
Ushirika vitaendelea kutoa ushirikiano na kuvitaka Vyama vya Ushirika
kuanzia ngazi ya Vyama vya msingi kutimiza wajibu wao Kiushirika kama
vile kuandaa makisio, kufanya mikutano mikuu ya mwaka pamoja na
kuhakikisha wanachama wanalipa hisa za chama. Hivyo, kuwezesha Chama
kikuu kufanya kazi vizuri na hatimaye mfumo wote wa Ushirika kutimiza
wajibu wake.
“Wanachama wa Ushirika ndio wamiliki
wa Vyama vya Ushirika hivyo viongozi wa Ushirika mnawajibika kwa
wanachama wenu kuhakikisha mnatoa taarifa za utendaji, taarifa za fedha
na maendeleo ya Vyama kupitia mikutano pamoja na matakwa mengine ya
Sheria ya Vyama vya Ushirka Na.6 ya mwaka 2013,” alisema Mrajis
Aidha amewataka wajumbe wa Mkutano
kusoma taarifa zinazotolewa na kuhoji pale inapobidi kuhusu masuala ya
uendeshaji wa Chama chao kwani Mkutano Mkuu ndio ngazi ya juu ya maamuzi
ya Chama
Hakikisheni mnafuatilia taarifa
zitakazoendelea katika Mkutano huu pale mnapoona hamridhiki mna haki ya
kuhoji, kupata majibu pamoja na kupitisha makisio na baada ya hapo
Mrajis Msaidizi wa Mkoa na Maafisa Ushirika wanaidhinisha kwa mujibu wa
Sheria.
Mrajis amewataka Viongozi wa Vyama vya
Ushirika kuwa wabunifu kwa kubuni miradi mbalimbali yenye tija na
maendeleo kwa Vyama vyao. Akiongeza kuwa ni muhimu Wanachama wa Ushirika
waweze kupata thamani ya kujivunia vyama vyao kupitia huduma za Vyama
zitakazowatofautisha wanachama na wasio wanachama wa Ushirika.
“Tuhakikishe kuwa ndani ya Vyama vya
Ushirika wakulima wanapata huduma bora kama vile upatikanaji wa pembejeo
kwa bei nafuu na kwa wakati, elimu ya ushirika, bima ya afya, masoko na
bei nzuri za mazao,” alisisitiza Mrajis
Mrajis ameeleza kuwa dhana ya Ushirika
ndio njia ya kuinua Uchumi wa watu wengi kwa pamoja hivyo ni muhimu
kuzingatia utendaji wenye kuzingatia maadili na taratibu za Ushirika ili
kulinda uendelevu wa Vyama na kujenga uchumi imara wa wananchi
wanyonge.
Dkt. Ndiege amevitaka Vyama vyote vya
Ushirika ambavyo vimepata hati chafu kwa mujibu wa Shirika la Ukaguzi wa
Vyama vya Ushirika (COASCO) kufanya jitihada mahususi za kuondokana na
dosari zilizosababisha hati hizo chafu. Alibainisha baadhi ya sababu za
hati hizo ni kukosa elimu ya uandishi wa vitabu, utunzaji mbovu wa
kumbukumbu na mengine.