Mazungumzo kati ya dpp na kigogo takukuru yakwama

Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, Kulthum Mansoor amedai
wameshindwa kufikia muafaka wa makubaliano baina yake na Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP).


Wakili
wa utetezi Elia Mwingira, alitoa madai hayo jana kwamba awali
walimwandikia DPP barua ya kuomba kukiri makosa yanayomkabili mshtakiwa,
lakini mazungumzo yamevunjika.

Alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Isaya.

Awali,
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo
ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado
haujakamilika.

Wakili wa utetezi Mwingira, alidai kuwa kwa kuwa mazungumzo na DPP yamevunjika upande wa Jamhuri uharakishe upelelezi.

Wakili Wankyo alidai wataelekeza wapelelezi kuhakikisha wanakamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobaki.

Hakimu Isaya alisema mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu na kesi hiyo itatajwa Januari 20, mwaka huu.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. bilioni 1.477.