Wazalishaji wa matofali ya kuchoma watakiwa kuzalisha matofali yanayokidhi

 

NA EMMANUEL MBATILO

Wazalishaji wa Matofali ya Kuchoma
wameshauriwa kuzalisha matofali yanayokidhi viwango ili kuweza
kuwanufaisha watumiaji na kuepuka madhara yatakayojitokeza.

Akizungumza na mwandishi wetu hivi
karibuni, Afisa Viwango Kitengo cha Ujenzi Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), Mhandisi Aziz Abdalah amesema kiwango cha utengenezaji wa
matofauli ni cha lazima kwahiyo mzalishaji analazimika kwa mujibu wa
sheria kuhakikisha anazalisha matofali yanayokidhi viwango vya ubora.

“Mzalishaji wa matofali ya kuchoma
kama amezalisha matofali ambayo hayajakidhi viwango basi kimsingi
atakuwa amefanya kosa kwa mujibu wa sheria”.Amesema Mhandisi Aziz.

Aidha Mhandisi Aziz amesema kuna
uimara wa tofali unatokana na udongo hivyo kuna udongo ambao haufai kwa
matumizi ya matofali na pia kuna udongo ambao unafaa kwa matumizi ya
matofali

“Kuna changamoto ya tofali
kubanduka ile inatokana na udongo uliotumika kuna udongo mwingine
unakuta una chumvichumvi sasa zile chumvichumvi zinapokutana na
unyevuvyevu, chumvi inatabia ya kufyonza unyevunyevu na kusababisha
tofali kubanduka”.

Hata hivyo Mhandisi Aziz amesema
ili wazalishaji waweze kujiridhisha na ubora wa matofali ambayo
wanazalisha wanatakiwa kufika kwenye ofisi za Shirika la Viwango
Tanzania na kuweza kuhudumiwa.

Pamoja na hayo Mhandisi Aziz
amesema Kiwango cha Matofali ya kuchoma kimeelezea hasa mambo mbalimbali
ikiwemo aina ya matofali ambayo yamegawanyika katika makundi manne
ambayo ni matofali ya kawaida,Matofali ambayo yanauwezo mdogo wa
kufyonza maji,Matofali ambayo yanatumika kwenye uhitaji wa uimara zaidi
na Matofali ambayo haitaji muonekano mzuri.