Dkt.abbasi asisitiza mageuzi ya kiutendaji kwa menejimenti

Na Anitha Jonas – WHUSM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan
Abbasi amewataka viongozi wa menejimenti wa Wizara hiyo kufanya mageuzi
kwa kuwa sekta za wizara  hiyo zimebeba ushawishi mkubwa kwa nchi  na
dunia.


Dkt.Abbasi ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma baada kuwasili katika ofisi
ya wizara hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba na kufanya mazungumzo na
viongozi wa Menejimenti kwa lengo la kupata taarifa fupi ya kisekta na
makabidhiano ya ofisi.


“Wizara hii imebeba sekta muhimu sana katika nchi ambazo ni soft power
na smart power mfano sekta ya Sanaa na Michezo ni burudani na sekta hizi
zikisimamiwa vizuri taifa hili litazidi kuwa la amani  na furaha pamoja
na uchumi utaongezeka,tutaandaa matamasha ya kitaifa ya burudani kama
JAMAFEST ambayo yatashirikisha wasanii na wachezaji sisi ni watumishi wa
umma lazima tuoneshe wananchi utendaji wetu na ningependa tuache
kufanya kazi kwa mazoea,”alisema Dkt.Abbasi.


 Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho, Dkt. Abbasi alisema kuwa
anatarajia kuona utendaji wa pamoja (team work) na utendaji wa kujituma
pasipo kuchoka,pia alisisitiza anategemea kutumia vipaji na ubunifu.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,
Dkt. Ally Possi alipokuwa akifanya makabidhiano alimweleza Dkt. Abbasi
changamoto mbalimbali za wizara ikiwemo ya uhaba wa fedha katika
uendeshaji wa Uwanja wa Taifa na pamoja na Programu ya Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika kuwa na changamoto katika uendeshaji, umuhimu
wa  programu hiyo sababu kuwa ni ya kimataifa na faida zake
utakaposimamiwa vyema na kukamilika.


“Nakupongeza kwa mapinduzi makubwa unayoyafanya katika Idara ya Habari
hakika kazi ni nzuri haswa katika kuisemea Serikali ningeomba kwa upande
wa usimamizi wa taaluma ya habari na Vitengo vya Mawasiliano Serikalini
huko nako nguvu inahitajika ili kuwa na utendaji wenye usawa katika
uwajibikaji wenye tija,’’alisema Dkt.Possi.


Aidha, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw.Marceline Patrick
alimpongeza Katibu Mkuu huyo na kumweleza kuwa watumishi wote
wamefurahia uteuzi wake na wana imani nae katika kusimamia mabadiliko ya
sekta za wizara na wapo tayari kumpa ushirikiano ili kufanikisha hilo.


Halikadhalika  mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo kutoka Idara ya
Maendeleo ya Utamaduni, Bibi Hadija Kisubi alisema anamshukuru
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt.John Pombe Magufuli kwa
kumteua Dkt.Abbasi kuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo sababu ni
mchapakazi na anaamini kuwa atafanya mabadiliko makubwa katika wizara
katika maeneo yote yenye changamoto.