Marekani yamaliza mafunzo ya kijeshi na kukabidhi vifaa kwa jwtz

Kaimu
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Inmi Patterson amekabidhi
vifaa mbalimbali vyenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 18 (Tsh
bilioni 41.6) kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kama sehemu ya
Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Afrika (African Peacekeeping Rapid
Reaction Program – APRRP).



Ubia
wa Majeshi ya Kulinda Amani ya Afrika (APRRP), ni ubia kati ya Marekani
na nchi sita za Afrika ambazo ni Tanzania, Uganda, Rwanda, Ethiopia,
Senegal na Ghana wenye lengo la kujenga uwezo na utayari wa kutoa msaada
wa kiuongozi na vifaa kwa oparesheni za kulinda amani za Umoja wa
Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU).

Katika
kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wakufunzi wa Kimarekani wamekuwa
wakifanya kazi na kikosi cha JWTZ ambacho ni sehemu ya Kikosi cha
Kimataifa cha Kulinda Amani ili kukijengea uwezo wa kushiriki katika
operesheni za kulinda amani, utoaji misaada ya kibinadamu na huduma
wakati wa majanga iwe nchini Tanzania na barani kote.

“Marekani
itaendelea kuwa mbia imara wa JWTZ,” amesema Patterson katika hafla ya
makabidhiano, na kuongeza kuwa “tutaendelea kuisaidia APRRP pamoja na
mafunzo ya awali ya askari walinda amani wa Kitanzania.”