Kesi ya erick kabendera yapigwa kalenda hadi februari 10

Upande
wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili, mwandishi wa
Habari za uchunguzi Erick Kabendera, umeieleza Mahakama ya hakimu Mkazi
Kisutu kuwa, mchakato wa makubaliano kati ya Kabendera na Mkurugenzi wa
Mashtaka nchini (DPP) bado unaendelea.

Wakili wa Serikali Gloria Mwenda amedai hayo leo Januari 27,2020 Mbele
ya Hakimu Mkazi, Jenet Mtega wakati kesi hiyo ilipokuja mahakamani hapo
kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mwenda amedai upelelezi bado unaendelea na mchakato wa
makubaliano kwa DPP pia unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa
ajili ya kutajwa.

 Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 10 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi hiyo, Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la utakatishaji wa Sh.Mil 173.

Kwa
mara ya kwanza Kabendera alifikishwa mahakamani hapo Agosti 5, 2019
akikabiliwa na makosa hayo anayodaiwa kuyafanya kati ya Januari 2015 na
Julai 2019, jijini Dar es Salaam.