Watoto 404 wafanyiwa ukatili wa kingono iringa

Na Mwandishi Wetu Iringa

Mkoa
wa Iringa kwa kipindi cha Januari mpaka Novemba 2019 umekuwa na matukio
takribani 404 ya vitendo ya ukatili wa kingono kwa watoto ikiwa ni
tatizo kubwa linalowakabili watoto katika malezi na makuzi yao nchini.

Hayo
yamebainika mkoani Iringa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Afya,
Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile
alipotembelea vikundi vya malezi kwa watoto katika kijiji cha Kising’a
kilichopo Wilaya ya iirnga mkoani Iringa.

Akitoa
taarifa hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Iringa Bi. Saida Mgeni amesema kuwa mkoa wa Iringa unakabiliwa na
matatizo mbalimbali na umekuwa ukiongoza katika masuala mabalimbali
yasiyofaaa katika jamii ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ameongeza
kuwa Serikali ya mkoa wa Iringa imejipanga katika kuhakikisha
inapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na
watoto mkoani humo kwa kuhakikisha inaratibu utoaji wa elimu kwa
wananchi juu ya madhara ya vitendo hivyo kwa wanawake na watoto.

Akizungumza
katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali haijalala
wala kufumbia macho suala la vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya
wanawake na watoto bali inachukua hatua kali kwa wahusika wa vitendo
hivyo wanaobainika.

Dkt.
Ndugulile amezitaka Kamati za malezi ya mtoto mkoani Iringa na nchi
nzima kuhakikisha wanatoa taarifa za vitendo vya kikatili dhidi ya
wanawake na watoto kwa kuhakikisha hawawafichi watuhumiwa na
hawamalizani kifamilia kesi za ukatil wa kijinsia.

Ameongeza
kuwa ni jambo la aibu kwa Tanzania ya viwanda kuwa na vitendo vya
kikatili kutokea katika jamii zetu kwani ni kikwazo kikubwa katika
kuhakikisha jamii inajiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

“Mkiona
wanajamii miongoni mwenu wanataka kumalizana katika kesi za vitendo vya
ukatili wa kijinsia toeni taarifa ili tukomehse vitendo hivi
visiendelee nchini” alisema Dkt. Ndugulile

Dkt.
Ndugulile amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanakaa na
kuzungumza na watoto wao na sio kuwapiga na kuwapa adhabu
zinatazosababisha kupata ukatili wa kisaikilojia ambao ni hatari kwa
malezi na makuzi yao na kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao za
msingi zilizopo kisheria.