Serikali yapokea gawio la sh. bilioni 8.7 kutoka kwa mashirika na taasisi za umma

Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma

Serikali
imepokea gawio na michango ya Sh. bilioni 8.7 kutoka kwa baadhi ya
Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma, ikiwa zimebaki siku 15 kati ya
siku 60 zilizotolewa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, za
kuzitaka Taasisi, Kampuni na Mashirika hayo kutoa gawio kwa Serikali.

Gawio
hilo limepokelewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango
katika hafla iliyowakutanisha Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za
Umma 13, jijini Dodoma.

Dkt.
Mpango amewaagiza, Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi, Kampuni na
Mashirika ya Umma ambao hawatatoa gawio ifikapo Januari, 23 saa sita
usiku kujiondoa katika nafasi zao na wasisubiri barua.

Alisema
kuwa ni vema kuhakikisha watu waliopewa dhamana katika Taasisi na
Mashirika ya Umma wanatumia rasilimali zilizopo katika kuiwezesha
Serikali kujitegemea kuliko kutegemea wafadhili ambao kwa sasa
wanapeleka nguvu kubwa katika nchi zao.

“Nawahakikishia
kuwa fedha hizi zilizopokelewa katika Mfuko Mkuu wa Hazina zitatumika
kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi masikini kwa kuwa Taasisi za
umma zilianzishwa ili uwekezaji wake uwanufaishe wananchi na Taifa kwa
ujumla”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt.
Mpango amezishukuru Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma kwa kutii
agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Novemba 24, 2019
lililozitaka taasisi hizo kutoa gawio ndani ya siku 60.

Alisema
kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liliingia ubia na Kampuni ya
Star Media ya China kwa kipindi cha miaka kumi na kwa mara ya kwanza
Kampuni hiyo imetoa gawio kwa Serikali la kiasi cha Sh. milioni 500,
jambo ambalo linapaswa kusifiwa hasa kwa uongozi wa TBC ulio saidia
kufanikisha jambo hilo.

Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji,
alisema kuwa ongezeko la maduhuli na michango kutoka kwenye Taasisi za
umma kwa zaidi ya asilimia 552, sio jambo dogo na inatoa tafsiri kwa
ulimwengu kuwa Tanzania sio masikini na sasa imeamua kusimamia
rasilimali zake.

Alisema
kuwa ni muda wa kuwaambia wananchi kuwa ni wakati wa kufaidika na fedha
zao za ndani ambazo Serikali yao iliwekeza kwa kuwa Rais ameamua
kutumia rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo ya watanzania.

Naye
Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, alisema kuwa kati ya Taasisi
187 ambazo hazikutoa gawio na michango kabla ya agizo la Rais la Novemba
24 mwaka jana, tayari Taasisi 151 zimetoa gawio na michango hiyo hadi
kufikia Januari 7, 2020.

Alisema
kuwa mpaka sasa jumla ya Sh. bilioni 20.8 zimepokelewa katika Mfuko
Mkuu wa Hazina, ambapo awamu ya kwanza katika kipindi cha kuanzia
Novemba 25 hadi Disemba 11, zilipokelewa Sh. bilioni 12.1 na awamu ya
pili kuanzia Disemba 12 mwaka jana hadi Januari 7 mwaka huu zimepokelewa
Sh. bilioni 8.7.

Bw.
Mbuttuka, alisema kuwa taasisi ambazo bado hazijatoa gawio na michango
ni 36, hivyo kuzitaka kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais la kutoa
gawio hilo kwa kuwa ifikapo Januari, 23, 2020 saa sita usiku  Wenyeviti
wa Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma
wasiotekeleza hawatakiwi kuingia ofisini.

Miongoni
mwa Taasisi zilizowasilisha gawio na michango ni pamoja na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania, Chuo cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Star Media, Bodi ya Utalii, Shirika
la Maendeleo la Taifa na Bodi ya Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi
(PSPTB).

Zaidi
ya Sh. trillion 1.2 zimekusanywa kutoka katika Taasisi, Kampuni na
Mashirika ya Umma 230 ikiwa ni gawio na michango mbalimbali kuanzia
Novemba 24 mwaka jana hadi Januari 7, mwaka huu.

Mwisho.