Nyoka aua askari wa wanyamapori kitanda

Na
Yeremias Ngerangera – Namtumbo

Askari msaidizi wa wanyamapori (VGS) wa kijiji cha Kitanda Wilayani
Namtumbo mkoani Ruvuma Halfani Mwale amefariki dunia baada ya kung’atwa
na nyoka muda mfupi baada ya tukio hilo.
Tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili ya tarehe 29 Desemba 2019 ambapo
marehemu na askari wenzake walikuwa doria katika pori la wanyama la
Jumuiya ya Mbarang’andu linalomilikiwa na vijiji kumi vya wilaya ya
Namtumbo.
Mtendaji wa kijiji cha kitanda bwana Ayubu Muhuwa alisema marehemu
alikutwa na mauti baada ya kukimbizwa kituo cha afya Namtumbo na
alipofikishwa kituo cha afya Namtumbo hali haikuwa nzuri na kutakiwa
kumfikisha hospitali ya rufaa ya Mkoa Ruvuma na kabla ya kufika
hospitali hiyo marehemu alifariki dunia.
Kwa mujibu wa maelezo ya askari mwenzake bwana Rashidi Maramae alidai
marehemu amefariki dunia kutokana na kuchelewa kupata huduma ya matibabu
kwani eneo alilong’atwa na nyoka haifiki pikipiki wala gari hali
iliyowapelekea kumpatia huduma ya kwanza kwa kumfunga kamba na kumbeba
kwenye machela mwendo wa masaa manne kwa haraka na kufika eneo
linalowezekana kupata usafiri.
Bwana Maramae alisema mara baada ya kufika eneo linalopitika kwa gari
walipiga simu kwenye uongozi wa Jumuiya na kutumwa gari ya kumbeba
marehemu lakini muda uliotumika toka marehemu alipong’atwa na nyoka saa
nane mchana ambapo wao walitembea kwa miguu kumbeba marehemu na kufika
eneo linalofika gari ulikuwa muda wa saa 11 jioni na gari ilikuja muda
wa takribani saa moja ya usiku hali hiyo ilichelewesha marehemu kupata
matibabu alisema Maramae.
Sefu Ndomondo na Joji Nditi askari wasaidizi wa wanyamapori kutoka
katika kijiji cha Nambecha walidai kazi hiyo ni ngumu lakini hawapati
mshahara wowote na kuongeza kuwa kitendo cha kuona mazingira aliyofia
mwenzao wamepata funzo juu ya kazi hiyo.
Askari wasaidizi wa wanyamapori Wilayani Namtumbo wanalalamikia
kutolipwa mshahara licha ya kufanya kazi ngumu kuwafukuza wanyama
waharibifu na wanaotishia maisha ya jamii katika vijiji vinavyozunguka
jumuiya ya Mbarang’andu na kuwafanya wasifanye kazi zao binafsi za
kujiongezea kipatao katika familia zao