Watalii 450 kutoka israel wako nchni kutembelea vivutio vya utalii


Watalii zaidi ya 450 kutoka Israel
wamewasili nchini mwezi Desemba 2019 kwa ajili ya tembelea vivutio vya
kitalii vilivyoko kaskazini mwa Tanzania. Watalii hao wamekuja nchini
kwa kutumia ndege binafsi na za kawaida.


Kundi la kwanza la watalii 150
liliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) tarehe 21 Desemba
2019 na kupokelewa na Bodi ya Utalii nchini (TTB) na baadaye kuelekea
katika vivutio vya utalii vilivyoko mkoani Arusha.


Kundi la pili na la tatu lililokuwa na watalii 305 limewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege KIA  tarehe 24 Desemba 2019.


Watalii hao wako nchini kwa ajili
ya kusherehekea sikukuu za Krismass na Mwaka mpya wanatembelea Hifadhi
za Taifa za Serengeti, Tarangire, Ziwa Manyara, Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorogoro na Bonde la Eyasi.


Ubalozi wa Tanzania nchini Israel
umetoa viza zaidi ya 500 kwa Waisrael ambao wamepanga kuwasili nchini
kwa kutumia Mashirika ya Ndege ya Ethiopia, Uturuki na Uswisi katika
kipindi hiki cha siku kuu za mwisho wa mwaka  huku ukiendelea kuratibu
ziara nyingine ya watalii zaidi ya 800 ambao mchakato wa safari yao upo
katika hatua za mwisho.


Ujio wa watalii hao unatokana na
jitihada za kuvutia watalii zinazofanywa na Ofisi ya Ubalozi nchini
Israel kwa kushirikiana na makampuni ya wakala wa utalii ya ndani na nje
ya nchi ili kuunga mkono harakati za Serikali za kukuza pato la taifa
kupitia utalii na hivyo kuiletea nchi maendeleo.