Wanaume shinyanga wakiri kuuza mazao kufanya ngono na wanawake weupe

Peter Shilinde maarufu ‘Ndizi/Banana’ akitoa ushuhuda jinsi alivyokuwa anauza mazao nyumbani na kwenda kununua wanawake weupe.
Chapa Mamba akitoa ushuhuda jinsi alivyokuwa anauza mazao nyumbani na kwenda kununua wanawake.

Na Marco Maduhu – Shinyanga

Baadhi ya wanaume wa kijiji cha Butini Kata ya Itwangi Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga wamekiri kuuza mazao ili kununua ngono kutoka kwa
wanawake (Makahaba), ambao hutoka mijini kwenye kipindi cha mavuno na
kwenda vijijini kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono ili kuchuma fedha
za mavuno kutoka kwa wanaume wa kijiji hicho.
Wamedai kuwa kinapofika kipindi cha mavuno ya mazao hua kuna ongezeko la
wanawake wengi weupe kutoka mjini, ambao hufika kijijini humo kwa ajili
ya kufanya biashara ya kuuza ngono, ambapo baadhi yao hushawishika na
kuamua kuuza mazao na kumpatia fedha mwanamke ambaye amempenda na
kushiriki naye ngono.
Mmoja wa wanaume kijijini hapo Peter Shilinde maarufu ‘Ndizi/Banana’
ambaye ana watoto wanne, ametoa ushuhuda kwenye maadhimisho ya siku 16
za kupinga ukatili wa kijinsia
yaliyofanyika Desemba 11,2019 yaliyoandaliwa na Shirika la Kivulini
ambalo linatetea haki za wanawake, kuwa yeye ni miongoni mwa wanaume
ambao walikuwa wakinunua makahaba kutoka mjini lakini sasa ameachana na
tabia hiyo.
Amesema kutokana na makahaba hao kuhitaji fedha nyingi ili wafanye nao
mapenzi, kuanzia shilingi 80,000 hadi 100,000, iliwalazimu kuuza mazao
yao ya mpunga na kuwapatia fedha hizo ambazo wanazihitaji na kisha
kushiriki nao ngono na kama mwanaume hana fedha itabidi ampatie gunia
zima la mpunga.
“Kuna tatizo kubwa hapa kijijini kwetu la wanaume kuuza mazao na kwenda
kununua ngono kwa makahaba ambao huja vijijini kufanya biashara hiyo
kwenye kipindi cha msimu wa mavuno, na mimi nilikuwa ni miongoni mwao
lakini nimeshaacha baada ya kuona nazidi kuwa maskini tu,” amesema
Shilinde.
“Na wanaume ambao hua wananunua mahakahaba ni wale ambao wanaendekeza
masuala ya ulevi, na ukiuza tu mazao unaikimbia familia na kuhamia
Sentani kwa muda wa siku mbili au tatu kwenye maeneo ambayo wanaishi
makahaba hao, fedha zikiisha unarudi nyumbani kuuza tena mazao
mengine”alisema.
Naye Chapa Mamba alisema kutokana na elimu aliyoipata kupitia shirika la
Kivulini alishaacha kuuza mazao nyumbani na kubainisha kuwa vitendo
hivyo vinachangia ukatili wa kijinsia.
Teleza Kazilo ambaye ni mhanga wa matukio hayo, amesema mume wake
alikuwa na tabia hiyo ya kuuza mazao na kwenda kununua ngono kwa
mahakaba wa mjini, na alipokuwa akipinga kitendo hicho alikuwa
akiambulia kipigo hadi chakula kinaisha ndani, na kuamua kwenda kufanya
vibarua ili watoto wapate chakula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Masanja Ikingo na Mtendaji wa
Kata ya Itwangi Claudia Kimaro, kwa nyakati tofauti wamekiri kuwepo na
vitendo hivyo na kubainisha lakini wameshindwa namna ya kuwadhibiti
makahaba hao ikiwa hua wanakwenda na njia ya kufanya biashara ya kuuza
Pombe ama kununua mpunga.
Aidha Ofisa Tathimini na ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini, Godfley
Paschal, amesema kijiji hicho cha Butini ni miongoni mwa vijiji
vilivyopo kwenye Kata ya Itwangi, ambavyo vinapewa elimu ya kutokomeza
matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo hali ya kiuchumi kwa wanaume
kuuza mazao yote na kununua ngono.