Atupwa jela miaka 30 kwa kumbaka bibi wa miaka 60

Mahakama
ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, imemuhukumu mkazi wa Kijiji cha
Nange, Shabo Marando (47) kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka bibi
wa miaka 60.


Mahakama
hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi Esther Malick, ilitoa hukumu hiyo baada
ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.

Malick
akisoma hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 87 ya mwaka 2019, akichambua
ushahidi wa shahidi wa tatu, Dk Judith  Kiwango wa hospital ya wilaya,
ambaye alimfanyia uchunguzi bibi huyo, alisema alimkuta na michubuko
sehemu za siri pamoja na manii.

Shahidi
wa pili ambaye ni Sama Luheka (34), mkazi wa Kitongoji cha Igokelo,
Kijiji cha Nange, alisema Julai 9 mwaka huu huko Igokelo baada ya
kusikia kelele katika vichaka alikwenda eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa
akimbaka bibi huyo.

Naye bibi huyo aliyebakwa, kwenye ushahidi wake alidai kuwa anamfahamu mtuhumiwa kuwa ni mkazi wa kijijini kwake.

Alidai
siku ya tukio alikuwa shambani akikusanya kuni na mtuhumiwa alifika na
kusalimiana na mara akamkamata kwa nguvu na kumvutia kichakani na
kumbaka.

Katika
utetezi wake, mtuhumiwa huyo alidai kuwa mlalamikaji ni shemeji yake,
alimpa eneo la kulima na siku ya tukio alikamatwa na wananchi baada ya
kuwa amechota maji ya kumwagilia nyanya zake kwa madai kwamba dimbwi
alilochota maji lilishazuiwa na kwamba si kweli kwamba alimbaka shemeji
yake.