Waaswa kulinda amani, masheikhe 20 wakihudhuria maulidi ya mtume muhammad s.a.w

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani
Kabeke (katikati),akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa BAKWATA wa
kupokea taarifa ya maandalizi ya sherehe za Maulidi ya Kitaifa
yanayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza Novemba 9, mwaka huu.


Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi
ya Mtume Muhammad S.A.W. Sadiki Mshola akitoa taarifa fupi ya fedha za
maandalizi kutoka vyanzo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa
Miundombinu na  Mapambo, Musa Mkumbi, akitoa taarifa kwenye mkutano Mkuu
Maalum wa BAKWATA mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhusu hatua iliyofikiwa
pamoja na bajeti inayohitajika.
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAUMINI wa Dini ya Kiislamu Jiji la
Mwanza wameaswa kulinda amani, utulivu na usalama wa nchi pamoja na
wageni wakati wote wa sherehe za Maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W, kwani
amani ikivunjika wote watahusika.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti
wa Masheikhe wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Haruna Kichwabuta, kwenye
Mkutano Mkuu Maalumu wa BAKWATA kwa niaba na masheikhe hao wakati wa
kupokea taarifa ya maandalizi ya maulidi uliofanyika,kwenye Ukumbi wa
Sheikhe Salum Ferej.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Kagera, alisema
suala la amani na utulivu ni muhimu, lakini ikivunjika waislamu wote
watahusika,hivyo lazima wajichunguze na kuwachunguza wengine wenye nia
ovu wanaoweza kujipenyeza ili kuvuruga amani, utulivu ili kuharibu jina
la Uislamu na Maulidi yenyewe.
 “Waislamu tuhakikishe tunakuwa macho
na watu wenye nia ovu wanaoweza kujipenyeza miongoni mwetu wakati wa
Maulidi ili kuchafua Uislamu.Tunahitaji watu watakaokuja hapa watusaidie
kulinda amani na utulivu wa nchi yetu na kuhakikisha usalama
unakuwepo.Pia tutakuwa na wageni , tuwaangalie na kusimamia usalama wao
licha ya kuwepo kwa vyombo vya ulinzi na usalama,”alisema Sheikhe
Kichwabuta.
Alisisitiza kwa vile waislamu wanayo
dhamana kubwa ya kulinda amani na utulivu wahakikishe sherehe hizo za
kihistoria za maulidi ya Mtume S.A.W. yanafanyika kwa amani, usalama,
mshikamano na upendo miongoni mwa waumini Kiislamu na jamii ya
Watanzania.
Sheikhe Kichwabuta pia ahimiza waumini
kushiriki na masheikhe kuendelea kusema na kukutangaza jambo hilo la
heri kwenye mimbari (msikitini) na kushughulika na watu wanaoyahitaji
maulidi,waachane na wasiyoyataka ili mwisho wa siku yafanyike kulingana
na hadhi ya Jiji la Mwanza.
Aidha, Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza alhaji
Hasani Kabeke alisema Kitendo cha Mufti Abubakar Zuberi kuipa BAKWATA
mkoani humu jukumu la kuandaa Maulidi ya Mtume S.A.W. Kitaifa baada ya
miaka 29 ni mtihani, ili kuufaulu ni kuyafanikisha.
Alisema kwa sababu Watanzania waislamu
na wasio waislamu wanashirikiana kwa mambo mbalimbali ya kijamii,
washirikiane kwa wenye uwezo,wajitoe hali na mali, wenye magari ama
nyumba za wageni wasaidie kuwahifadhi wageni hao wa Mtume S.A.W. na
kuwasafirisha.
Tunashirikiana na waislamu na wasio
waislamu, hivyo wasio waislamu hawajaweewa pazia (mipaka), wanayo haki
ya kuchangia Maulidi.Wajitokeze na watusaidie kuwahudumia wageni wa
Mtume Muhammad S.A.W. na si BAKWATA.Watakachotoa ni kwa ajili ya wageni
hao wa mtume,”alisema.
Kwa mujibu wa Sheikhe Kabeke jumla ya
watu 10,000 wanaratajiwa kuhudhuria kwenye sherehe hizo wakiwemo
masheikhe 20 kutoka nchi za Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda, kuanzia
Novemba 4 hadi 9, mwaka huu  huku shilingi milioni 171 zihitajika kwa shughuli hiyo.