Dkt. kijaji aipa tra siku 75 kuandaa orodha kamili ya walipakodi, majengo na mabango

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameipa Mamlaka ya Mapato
Tanzania TRA miezi miwili na nusu hadi ifikapo Disemba 31 mwaka 2019,
kuandaa na kuwasilisha wizarani orodha ya walipakodi, idadi ya majengo
na mabango yote yaliyoko katika mkoa wa Dar es Salaam ili kupata
takwimu sahihi za idadi ya walipakodi. 

Dkt.
Kijaji ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi
katika Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke ili
kukagua utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hayo ili kubaini fursa na
changamoto za masuala ya ukusanyaji kodi.

Amesema
kuwa pamoja na Mamlaka hiyo kufanya vizuri katika makusanyo ya mapato
Mwezi Septemba, 2019, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.78
kimekusanywa, kiasi hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na mwamko wa
wananchi uliopo hivi sasa katika kulipa kodi.

Aidha
Mhe. Kijaji amerejea kuitaka TRA kuwasilisha kwake takwimu ya ongezeko
la walipa kodi lililotokana na zoezi la kugawa vitambulisho vya
wajasiriamali nchini kwa kuwa lengo la Mhe. Rais Dkt. John Magufuli
kugawa vitambulisho hivyo lilikuwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi
watakao kuwa wanafuzu kwa kuongeza mitaji yao, hivyo ni vyema kujua
idadi yao kamili na mahali walipo.

Kwa
upande wa kodi ya majengo, Dkt. Kijaji ameitaka Mamalaka ya Mapato
Tanzania kuhakikisha inapata orodha ya nyumba zote nchini kwa
kuorodhesha wamiliki wa nyumba hizo na mawasiliano yao na kisha kuandaa
kanzidata itakayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo. 

“Ili
kuongeza mapato yanayotokana na kodi ya majengo ni lazima TRA wafanye
kazi usiku na mchana kuhakikisha kanzidata hiyo inakamilika ambayo
itatumika kuwakumbusha walipa kodi kupitia ujumbe mfupi wa simu ambapo
itasaidia katika ukusanyaji wa kodi hiyo kama ilivyo kwa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inapowakumbusha wananchi kulipa
kodi a ardhi kupitia simu zao
” Alisema Dkt. Kijaji

“Nataka
pia mkague watumiaji wote wa mashine za utoaji risiti za kieletroniki
(EFD) kwa wafanyabiashara wa Temeke ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa
risiti na anayenunua anadai risiti na kwa kufanya hivyo itasaidia
kuongeza makusanyo ili Taifa liendelee kujitegemea kimapato” alisisitiza
Dkt. Kijaji 

Awali
akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Meneja wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Bw. Paul Walalaze, alisema
mkoa wake una idadi ya walipakodi 437,539 na kwamba katika mwaka
2018/19, mkoa wake ulipanga kukusanya shilingi bilioni 395 na kufanikiwa
kukusanya sh. bilioni 328.5 sawa na asilimia 85 ya lengo.

“Tumekusanya
pia kodi ya majengo sh. bilioni 1.4 kati ya malengo ya kukusanya
bilioni 1.6, kodi ya mabango sh. bilioni 2.2 kati ya lengo la kukusanya
sh. bilioni 2.3 sawa na mafanikio ya asilimia kati ya 87 na asilimia 95″
aliongeza Bw. Walalaze.

Kwa
upande wake Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw.
Hamisi Lupenja, amemhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Kijaji kwamba watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuboresha
ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwemo kutoa elimu kwa walipakodi.
 Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), katikati, akikagua
kanzidata ya walipakodi wa majengo na mabango, katika Ofisi za Mamlaka
ya Mapato Tanzania-TRA, mkoa wa Kikodi wa Temeke Jijini Dar es Salaam.
Kulia ni Bi. Hellen Gibbe Msimamizi Msaidizi wa Kodi na kushoto ni
Msimamizi wa Kitengo cha Mapato yasiyo ya Kodi, wote kutoka TRA-Temeke.
 Mkuu
wa masuala ya usimamizi wa Data na Ukaguzi wa ritani Bw. Pius Kunjumu
(aliyesimama nyuma) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango (Hayupo pichani) alipofanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam,
kusikiliza fursa na changamoto ya utendaji kazi wa Mamlaka hayo ili
kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi.
 Meneja
Msaidizi wa Kitengo cha Madeni wa TRA-Temeke, Bw. Nicholaus Migera,
(aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango (Hayupo pichani) alipofanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania-TRA Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam,
kusikiliza fursa na changamoto ya utendaji kazi wa Mamlaka hayo ili
kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi.
 Afisa
Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Hamisi Lupenja
akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi
hizo za TRA Mkoa wa Kikodi wa Temeke Jijini Dar es Salaam.
 Afisa
Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Hamisi Lupenja
(kulia) na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa
Temeke, Jijini Dar es Salaam. Bw. Paul Walalaze, wakisikiliza hoja za
watumishi wa TRA-Temeke, Jijini Dar es Salaam wakati Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipofanya
ziara ya kikazi katika Ofisi hizo.
 Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akisikiliza kwa
makini hoja mbalimbali za watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA
Ofisi ya Temeke (hawapo pichani), alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania-TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam
Katibu
wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Bw. Moses
Dulle, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo wakati Dkt. Kijaji aliofanya
ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania TRA, Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Jijini Dar es Salaam
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)