Serikali yavunja mkataba na mkandarasi ujenzi wa jengo la polisi manyara


Na Mwandishi Wetu

Serikali
imewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Manyara kuanza na kumalizika kwa
Mradi  Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi  ambao
ulisimama tangu mwaka 2012 kutokana na gharama kubwa ya ukandarasi na
sasa utajengwa kwa kutumia utaratibu mpya wa serikali wa nguvu mali
ambao utapunguza gharama za ujenzi kulinganisha na kutumia mkandarasi.


 Hayo yamesemwa leo  na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi
Hamad Masauni alipotembelea mradi huo uliopo katika eneo la Komoto Kata
ya Bagara Wilayani Babati Mkoani Manyara ambao gharama za awali za mradi
huo ni  Milioni Mia Tano Themanini na Moja,Laki tatu na Thelathini.
“Serikali tunawahakikishia wananchi wa Mkoa wa Manyara kujengwa kwa
jingo la polisi ili masuala ya ulinzi na usalama yaweze kuwa imara
katika mkoa huu,tayari timu maalumu kutoka makao makuu ya polisi
ilishafika hapa na kuona jinsi mradi huu utakavyoweza kuendelea baada ya
kusimama kwa takribani miaka saba sasa,” alisema Naibu Waziri Masauni
“Juhudi mbalimbali zishaanza na hivi navyozungumza tayari Jeshi la
polisi mkoani hapa likishirikiana na wadau wameshafanya harambee na
kufanikiwa  kukusanya  takribani  kiasi cha Shilingi Milioni Arobaini na
Tano na sisi kama Wizara tutachangia ujenzi huo” aliongeza Masauni
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo la mradi Mbunge wa Babati
Mjini Pauline Gekul alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi katika
mazingira madogo,ofisi ni ndogo hali inayopelekea huduma kutolewa kwa
uchache tofauti na mahitaji
“Nashukuru kuona serikali leo imefika kuona maendeleo ya huu mradi kwa
kweli polisi wanahitaji jingo jipya ili kazi ya kulinda amani na utulivu
iwe rahisi kwao,tunashukuru pia wadau mbalimbali wameanza kutuunga
mkono ikiwa pia na ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya askari wetu”
alisema Mbunge  Gekul
Awali akitoa taarifa ya Uhalifu Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Manyara,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Cyprian Mushi alikiri kupungua  kwa
uhalifu huku akikiri kuwepo changamoto katika kutatua baadhi ya kesi za
ubakaji baada ya familia za mtuhumiwa na familia ya mtuhumu kutotokea
mahakamani baada ya kuzimaliza kesi hizo kifamilia.