Dc mwaimu awatangazia kiama wanaohujumu miradi ya maendeleo kyerwa

Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Mh. Rashid Mwaimu

Na Lydia Lugakila – Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera Mhe. Rashid Mwaimu 
amesema atapambana vikali usiku na mchana ili kuhakikisha anakomesha
watu wanaotaka kuhujumu miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi
itolewayo na serikali akibainisha kuwa yupo tayari kukesha katika maeneo
yote ya miradi ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya hiyo Rashid Mwaimu ametoa kauli hiyo Septemba
27.2019 ofisini kwake wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu
miradi ya maendeleo wilayani hapo.
Mhe.Rashid amesema atahakikisha analinda na kusimamia miradi mbalimbali
ya maendeleo inayoletwa na serikali wilayani humo huku akiahidi
kuwashughulikilia wale wanaotaka kufanya vitendo vya kuihujumu serikali.

Amesema kutokana na jitihada, nguvu na
busara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli
katika utekelezaji wa miradi ya ki maendeleo yeye kama mkuu wa wilaya
hatomfumbia macho mtu yeyote anayepanga kuhujumu miradi hiyo.


“Nawaahidi miradi yote inayoletwa na serikali kwa ajili ya wilaya ya
Kyerwa nitaisimamia na kuilinda kwa nguvu zote, nitahakikisha adui
yeyote haisogelei miradi hiyo ,miradi ni mali ya wananchi ole wenu
mliozoea kuitafuna muda umekwisha, nitacheza na nyie usiku kucha”,
alisema Mwaimu.
Hata hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha
katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuwahimiza kutomchagua
kiongozi mbishi, badala yake wachague kiongozi ambaye ni mzalendo na
muadilifu atakayewaletea maendeleo.
Katika suala la ulinzi na usalama, amesema katika wilaya yake ulinzi na
usalama ni wa kutosha hivyo amewataka wananchi kuripoti katika vyombo
husika mara moja vinapojitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani kwa
baadhi ya watu wasiowaadilifu hasa katika kuelekea uchaguzi wa serikali
za mitaa.