Nimr yakutanisha wanasayansi, watafiti kujadili ukimwi arusha…serikali yasema kondom zipo zakutosha, tatizo ni usambazaji

NIMR YAKUTANISHA WANASAYANSI, WATAFITI KUJADILI UKIMWI ARUSHA -SERIKALI YASEMA KONDOM ZIPO ZAKUTOSHA, TATIZO NI USAMBAZAJI

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee,
jinsia, watoto na walemavu Dkt Faustine Ndugulile akifungua kongamano la
watafiti, wanasayansi na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ulioanza
leo jijini Arusha
.

Viongozi wa Taasisi za utafiti, wanasayansi na wadau wa
sekta ya afya wanaopambana na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi wakiwa katika
picha ya pamoja na Naibu waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee,
jinsia, watoto na walemavu Dkt Faustine Ndugulile wanne kutoka kulia aliyekaa.



Na Seif Mangwangi, Arusha


SERIKALI imesema bado inayo akiba ya kutosha ya mipira ya kujinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (Condom), na kwamba kinachoonekana kukosekana kwa mipira hiyo ni changamoto mpya ya kuisambaza tofauti na njia iliyokuwa ikitumika hapo mwanzo.


Hayo yameelezwa leo Septemba 10, 2019 na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na walemavu, Dkt Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kongamano la kitaifa lililoandaliwa na taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya Binaadam (NIMR).


Dkt Ndugulile amesema Serikali imekuwa kwenye mikakati kabambe ya kuhakikisha tatizo la ugonjwa wa Ukimwi linamalizwa ifikapo mwaka 2030 na kwamba kongamano hilo limekutanisha taasisi, watafiti na wadau mbalimbali kwaajili ya kubadilishana tafiti zao na kupanga mikakati ya kufikia malengo makuu ya kumaliza ugonjwa wa Ukimwi.


Amesema tafiti zinaonyesha kuwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi Serikali imekuwa ikiweka malengo mbalimbali kuhakikisha mpango wake wa hadi kufikia mwaka 2020 unafikia malengo iliyojiwekea ikiwemo kupunguza tatizo la maambukizi kwa asilimia tisini.


“Ili hizi asilimia tisini tatu ambayo moja wapo ni kujua idadi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, kupata watu wanaokwenda kupima kwa hiyari na kugawa dawa za kufubaza maambukizi ya ukimwi zinatimizwa Serikali imekuwa ikiweka mipango kabambe na hakika kwa mwendo tunaoenda nao tunatimiza maelngo yetu,”anasema.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee,
jinsia, watoto na walemavu Dkt Faustine Ndugulile akipata maelezo ya namna
taasisi ya AMREF inayopambana na maambukizi ya Ukimwi kwa njia ya vipimo na
kutoa elimu kwa jamii alipotembelea banda lao leo hii
.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee,
jinsia, watoto na walemavu Dkt Faustine Ndugulile akipata maelezo ya namna
taasisi ya NACOPHA inayopambana na maambukizi ya Ukimwi alipotembelea banda lao
leo hii, nyuma ya waziri ni Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya
binaadam NIMR Prf Yunus Mgaya


Mkurugenzi
Mkuu wa taasisi ya utafiti wa Magonjwa ya binaadam nchini (NIMR) Prf
Yunus Mgaya akitoa salamu za taasisi yake katika kongamano la kitaifa la
watafiti, wanasayansi na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi
nchini katika mkutano unaendelea jijini Arusha


Anasema pamoja na Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu kuanzisha mpango wa watu kujitokeza kupima kwa hiyari bado mango huo unaonekana kukwamishwa na wanaume ambao wamekuwa wagumu kujitokeza lakini wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi.
Dkt Ndugulile anasema kufikia Novemba Mwaka huu 2019, Serikali itakuwa imepeleka bungeni sheria itakayokuwa ikieleza mpango madhubuti wa watu kujitokeza kupima kwa hiyari na kwamba mpango huo utafanana na mpango wa wanawake kupima ujauzito kwa hiyari kupitia vipimo vinavyopatikana katika maduka ya dawa.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, jinsia,
watoto na walemavu Dkt Faustine Ndugulile akipata maelezo ya namna
taasisi ya THPS inavyopambana na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi
alipotembelea banda lao leo hii. Nyuma ya Waziri Ndugulile ni Prf Yunus
Mgaya Mkurugenzi wa taasisi ya NIMR.


Pia amesema takwimu zinaonyesha kuwa pamoja na idadi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kupungua kwa asilimia kubwa, maambukizi mapya ya Zaidi ya asilimia 40 yamekuwa yakitokea kwa vijana wadogo wa umri wa miaka 14 hususani wasichana.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya NIMR Profesa Yunus Mgaya amesema kupitia kongamano hilo wadau watajadili masuala mbalimbali yanayohusu utafiti wa ugonjwa wa Ukimwi na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kutekeleza mpango wa serikali wakutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.


Wakati huo huo, Naibu Waziri Dkt Ndugulile ameiagiza taasisi ya utafiti ya NIMR kutengeneza mpango wa utoaji wa matokeo ya utafiti wa magonjwa mbalimbali nchini ikiwemo ugonjwa wa Ukimwi badala ya kila taasisi kufanya tafiti na kutoa takwimu kulingana na matakwa ya taasisi yake.


Amesema ukifuatilia takwimu zinazotolewa na taasisi mbalimbali zinazofanya tafiti juu ya ugonjwa wa Ukimwi zimekuwa zikutofautiana jambo ambalo sio sahihi na kuagiza mpango huo usitishwe mara moja na taasisi ya NIMR iratibu utaratibu ambao utafanya tafiti hizo kuwa moja kote nchini.