Maafisa ugani watakiwa kutoa huduma ya kitaalamu kwa wananchi, kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji

 Na Mwandishi Wetu, APC BLOG, Kagera 

SERIKALI imewataka Maafisa Ugani nchini kutendea haki taaluma yao kwa kutoa huduma bora ya kitaalamu kwa wananchi wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ili kuwezesha upatikanaji wa maendeleo katika sekta hizo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipokuwa akifunga maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) katika viwanja vya Kyakailabwa mkoani Kagera.

Dkt. Mwanjelwa amewasisitiza Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanawafuata wananchi katika maeneo yao ya uzalishaji ili kuwapatia huduma ya kitaalamu kwa wakati badala ya kukaa ofisini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) mkoani
Kagera akiangalia chakula cha samaki katika bwawa la kufugia samaki la Jeshi la Magereza Kagera lililopo Viwanja vya Kyakailabwa mkoani Kagera.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) mkoani Kagera akiangalia mboga katika shamba darasa la Jeshi la Magereza lililopo Viwanja vya Kyakailabwa mkoani Kagera.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) mkoani Kagera akielekea kukagua mabanda ya maonyesho katika Viwanja vya Kyakailabwa mkoani Kagera. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) mkoani Kagera akitunuku cheti na zawadi kwa watumishi wa Kiwanda cha Sukari Kagera ambao ni washindi wa pili wa jumla wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima katika Viwanja vya Kyakailabwa mkoani Kagera.

Sanjari na hayo, Dkt. Mwanjelwa ametoa rai kwa wananchi kuzingatia kanuni za kilimo, uvuvi na ufugaji ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuondokana na gharama sizizo za lazima katika shughuli za uzalishaji.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka wananchi kutilia mkazo katika sekta ya kilimo kwani ndio inayobeba asilimia kubwa katika maendeleo ya viwanda.

“Kilimo ndio sekta wezeshi kwa uchumi wa viwanda, asilimia 80 ya viwanda vyetu inategemea malighafi ya kilimo hivyo ni lazima ipewe kipaumbele ili kufikia uchumi wa kati wa viwanda,”  Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Kauli Mbiu ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) mwaka huu ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi na maadhimisho ya kitaifa kwa mwaka huu yamefanyika mkoani Simiyu.

Dkt. Mwanjelwa amehitimisha kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) katika mkoa wa Kagera, akiwa kwenye ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.