Mamlaka ya mapato tanzania (tra) mkoa wa shinyanga yafanikiwa kukusanya kodi bilioni 32.8, walipa kodi wapewa zawadi na vyeti vya pongezi

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa
Shinyanga imefanikiwa kukusanya kodi kiasi cha shilingi Bilioni 32.8 sawa na
asilimia 82.21 ya lengo lililokusudiwa kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yameelezwa  na Naibu
mkurugenzi wa fedha TRA makao makuu Bi. Anna Mndeme kwenye kilele cha
maadhimisho ya siku ya shukurani kwa mlipa kodi iliyofanyika katika viwanja vya
zimamoto Nguzonane Manispaa ya Shinyanga

Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya
walipa kodi wazalendo na waandilifu wanaounga mkono juhudi za serikali katika
kusukuma maendeleo.

“Kwa
kuwa leo ni kilele cha maadhimisho ya siku ya shukurani nitumie nafasi hii
kutambua mchango mkubwa wa wateja wetu yaani walipa kodi na wadau mbalimbali
ambao ndiyo kipekee wanatuwezesha TRA Mkoa wa Shinyanga kufikia malengo ya
makusanyo ya kodi tuliyopewa na serikali”.

“Mwaka
wa fedha 2022/2023 mamlaka imefanikiwa kukusanya kodi kiasi ya cha Bilioni 32.8
ukusanyaji huu ni ufanisi wa asilimia 82.21 ya lengo la kukusanya ambalo
tulipewa Mwaka huo”.

Katika maadhimisho hayo TRA Mkoa wa
Shinyanga imewapongeza walipa kodi wote, kuwatambua na kuwatunuku vyeti na
zawadi mbalimbali walipa kodi na wadau wengine ambao wameonyesha mchango mkubwa
kwa mamlaka hiyo.

Afisa elimu na mawasiliano kwa mlipakodi
Semeni Mbeshi ametaja baadhi ya majira ya washindi wa tuzo hizo ambapo kituo
cha matangazo Radio Faraja FM kimeshinda tunzo katika nafasi ya chombo cha
habari kinachosaidia kueneza zaidi elimu ya kodi kwa wafanyabiashara Mkoa wa
Shinyanga.

 “Taasisi ya kwanza ambayo imeonyesha
ushirikiano na TRA ni ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ofisi nyingine ni
ofisi ya RSO , ofisi nyingine ni ofisi ya kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa
Shinyanga anayefuata ni vyombo vya habari 
ambavyo vimeweza kuwa msaada katika kueneza masuala ya yetu ya kodi ikiwemo
elimu ya kodi cheti kinaenda kwenye Redio ambayo inaitwa Redio Faraja”
.amesema
Semeni Mbeshi

Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Bwana
Faustine Mdessa  amesema  katika maadhimisho hayo mamlaka hiyo  yamekwenda sanjari na kutoa msaada  kwa watu wenye uhitaji ikiwemo kituo cha
wazee na wasiojiweza kolandoto pamoja na kutoa msaada wa Tenki la maji katika
Hospitali ya Wilaya ya Kishapu.

Akizungumza mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bi. Mboni Mhita ameipongeza TRA
Mkoa wa Shinyanga kwa kutambua mchango wa walipakodi huku akiwakumbusha walipakodi
kuendelea kulipa kodi kwa hiyari.

DC Mhita amewataka wafanyabiashara kutoa
lisiti kwa kutumia mashine sahihi za EFD wakati wa mauzo huku akiwakumbusha
wanunuzi kudai lisiti wakati wa kuchukua bidhaa kwa wafanyabishara hali
itakayosaidia kuziba mianya ya ubotevu wa fedha.

Mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga
Elias Ramadhan Masumbuko na Mwenyekiti wa TCCA Mkoa wa Shinyanga Jonathan
Manyama wamewaomba wakazi wa Mkoa wa Shinyanga  kuendelea kulipa kodi kwa hiyari.

Kauli mbiu ya
maadhimisho hayo ni ‘KODI YETU. MAENDELEO YETU. TUWAJIBIKE’.

Awali yakiendelea matembezi ya hiyari kwa
watumishi wa TRA, walipa kodi pamoja na wanafunzi wa klabu za kodi kutoka
katika shule na vyuo mbalimbali Mkoani Shinyanga.