Mahakama yatoa hati ya kukamatwa kwa jacob zuma

Mahakama ya juu ya Pietermaritzburg
nchini Afrika Kusini imetoa hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa nchi
hiyo, Jacob Zuma baada ya kushindwa kufika mahakamani kukabiliana na
mashtaka kuhusu rushwa dhidi yake.


Hati hiyo itafanya kazi ikiwa atashindwa
kuhudhuria kesi yake itakayoanza mwezi Mei. Bwana Zuma anakabiliwa na
makosa 16 ya kughushi, rushwa , ulaghai na utakatishaji fedha ukihusisha
biashara ya silaha ya thamani ya mabilioni ya dola iliyofanywa tangu
miaka ya 1990.

Rais huyo wa zamani amefanikiwa kukwepa
shutuma za rushwa dhidi yake kwa zaidi ya miaka 10. Lakini leo, sheria
haikuwa upande wake.

Hati ya kukamatwa kwake imetolewa baada
ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake. Jopo
la wanasheria wake waliwasilisha nyaraka wakisema kuwa mteja wao alikuwa
mgonjwa na amekuwa akipatiwa matibabu nje ya Afrika Kusini tangu mwezi
uliopita.

Jaji Dhaya Pillay alihoji maelezo yaliyo
kwenye nyaraka za matibabu za Zuma zilizowasilishwa na mawakili wake
mahakamani. Lakini rais huyo wa zamani atakamatwa ikiwa atashindwa
kufika mahakamani tarehe 6 mwezi Mei kesi yake itakapoanza rasmi.
Chanzo- BBC