MFANYABIASHARA WA NAFAKA MBINGA ALIA NA SOKO LA MAZAO

MFANYABIASHARA na mnunuzi wa mazao ya mahindi na Maharage, Agustino Njaku wa kijiji cha Mkako Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma amewashangaza wananchi na viongozi wa taasisi binafsi za serikali mkoani humo kwa kitendo cha kununua mahindi kwa bei ya juu  kisha yeye kuyauza kwa wafanyabiashara kwa bei  ya chini. Mwandishi Amon Mtega anaripoti kutoka Ruvuma 

  Mfanyabiashara huyo  amesema kuwa maamuzi hayo yamekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wakulima wa mahindi wa Kijiji cha Mkako kuwa mahindi yao yanakosa soko ambapo Serikali ilisitisha kununua mahindi badala yake wafanyabiashara walikuwa wananunua kwa shilingi 380 bei ambayo haikidhi gharama ya uendeshaji.

 Kutokana na adha hiyo kampuni yao ya  Njaku LTD iliamua kuanza kununua mahindi ya wakulima wa Kijiji cha Mkako ambapo kilo moja ya mahindi walinunua kwa sh. 600 wakati bei elekezi ya serikali sh. 500.

 Amesema kuwa wiki moja baadae wananchi wengi wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa mazao wenye mahindi yaliyokosa soko walimiminika kwenda Mkako kuuza mahindi yao.

Njaku amesema kuwa lengo la kununua mahindi hayo ni kumkwamua mkulima hivyo wameona ni vyema wakaongeza bei ya mahindi ambapo kutoka shilingi 600 hivi sasa kilo moja wananunua kwa sh. 750.

 Jambo lililowashangaza wananchi wengi wakiwemo baadhi ya viongozi ni kitendo cha mfanyabiashara huyo kununua mahindi kwa bei kubwa na wao wanayauza kwa wafanyabiashara wa mazao mchanganyiko wa SODECO kwa bei ya sh.380.

 Mfanyabiashara huyo amesema kuwa hawana soko maalumu wanalolitegemea la kuuzia mahindi wanayoyanunua kutoka kwa wakulima adhima yao ni kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara wadogo ambao wanauziwa kwa bei ndogo ambao wanayasafirisha nje ya mkoa na kwenda kuyauza kwa bei ya juu.

“Tulianza kama maradi mdogo tu wa kusaidia wananchi kwa kuwa pesa kidogo zilikuwepo za kuwasaidia wananchi ili waweze kuuza mahindi yao kwa kuwa wanapata shida sana hawajui mahindi yao watauzia wapi,tulianza kununua mahindi kwa gunia bila kupima kwa sh. 60,000 lenye ujazo wa kilo 135 na mpaka sasa mahindi yanakuja kwa wingi kama mnavyoona hapa.” Amesema  Njaku.

‘’Biashara hiyo ni endelevu japo kuwa kuna vikwazo ambavyo tunakutanana navyo ikiwemo baadhi ya mamalaka za serikali wanataka ushuru mala mbili wakati sisi lengo lao ni kusaidia wananchi’’Amesema.

 Wakizungumza  baadhi ya wakulima na wafanyabiashara waliotoka maeneo mbaimbali ndani ya wilaya hiyo na nje ya wilaya hiyo ndani ya mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye viwanja vya soko la mahindi Mkako wamesema kuwa mfanyabiashara huyo wanamfananisha na nabii ambaye ameshushwa na Mungu kuja kuwaokoa wakulima ambao  wamekuwa wakikosa soko la kuuza mazao yao kwa muda mrefu.

 Mmoja wa wafanyabiashara Pumziko Tony Blea amesema kuwa wamefurahishwa na soko hilo kwa sababu mazao yao yamekosa soko kwa muda mrefu jambo ambalo lingewakwamisha kiuchumi lakini uwepo wa soko hilo linajibu maswali ya muda mrefu waliokuwa wanajiuliza nini hatima ya mazao yao.

 Amesema kuwa kwa sasa serikali inatakiwa kumuunga mkono mfanyabiashara huyo kwani kuna baadhi ya taasisi za serikali zimeanza kumsumbua kwa kudai kodi mala mbili jambo ambalo linaweza kumkatisha tamaa na kuacha kununua mazao yao.

 Gress Kapinga ambaye ni mama lishe amesema kuwa kuibuka kwa mfanyabiashara huyo kwenye kijiji chao cha Mkako kimesaidia biashara yao kukuwa kwa haraka na kuongeza kipato kwani awali alikuwa anauwezo wa kuuza chakula kuanziaasubuhi hadi mchana lakini kwa sasa anauza hadi usiku.

 Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vijijini  Pascal Ndunguru alisema kuwa mfanyabiashara huyo ameomba kibali cha kununua tani za mahindi 1500 na tani 500 za maharage kibali ambacho kimetolewa Septemba 15 mwaka huu.

Amesema kuwa aliomba kununua katika vijiji vya Matiri,Lukalas,Kigonsera,Amani makoro,Rwanda pamoja na Mkako na kwamba toka kuwepo kwa mfanyabiashara huyo mapato yameongezeka na sasa wanampango kuweka miundombinu ikiwemo vyoo na maji safi na salama  ,huku akiwataka wananchi wa Wilaya hiyo kutafakari ubora wa soko wanalopeleka na wawe makini na si vinnginevyo.

MWISHO.