Aina mpya ya nafaka kusaidia kuondoa tatizo la kudumaa kwa watoto wadogo

 

 

Na Claud Gwandu,Arusha

 

UGUNDUZI wa aina mpya ya nafaka unaweza kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la kudumaa kwa watwenye umri wa chini ya miaka mitano iwapo wazazi watatumia nafaka hiyo kama sehemu ya chakula, imeelezwa

 

Nafaka hizo mpya zenye protini nyingi na zimegunduliwa katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI-Tengeru na zimepewa majina ya Poli na Akeri ambayo ni maaeneo maarufu kwa jamii zinazoishi chini ya Mlima Meru mkoani Arusha

 

Mtafiti kutoka katika kituo hicho, Alhaji Saidi anasema kuwa nafaka hizo pia zina vitami C, Vitamini A na madini aina ya calcium, magnesium, potassium, chuma na fosforasi ambayo ni madini muhimu katika makuzi ya mtoto

 

“Aina hii ya nafaka inaweza kuwekwa na kutumiwa katika uji hasa kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano,”anafafanua mtaalam huyo katika mafunzo ya wanahabari yaliyoandaliwa hivi karibuni na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jijini hapa

 

Mtaalam huyo alisema kwamba aina hizo mpya za nafaka zinaweza kuwa mbadala wa matumizi ya nyama yaliyokatazwa kwa baadhi ya watu kutokana na sababu za kitabibu

 

“ Ikiwa na protini nyingi na baadhi ya madini muhimu katika mwili, inaweza kutumika kama mbadala wa nyama kwa watu wenye changamoto za kiafya zinazozuia kula nyama,” alisema na kuongeza:

 

“ Tangu zilipogunduliwa mwaka 2019,nafaka hizo zimesaidia watoto wengi waliokuwa wanakabiliwa na matatizo ya kukua kutokana na sababu mbalimbali.”

 

Mtaalam mwingine wa kilimo katika Kituo cha kuzalisha mbegu za kilimo(ASA-Tengeru) alisema kwamba mahitaji ya aina hizo za nafaka yamekuwa makubwa sokoni kutokana na umuhimu wake katika lishe na kwamba makampuni zaidi ya 50 yamepeleka maombi ya kupewa nafaka hizo.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Lishe duniani ya mwaka 202, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kufikia malengo ya kuondoa udumavu kwa watoto, lakini asilimia 31.8 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano bado wanakabiliwa na matatizo hayo.