Arusha yajipanga kukomesha vitendo vya kihuni maadili mashuleni

Na Magesa Magesa,Arusha

SERIKALI Mkoani Arusha imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa inakabiliana na vitendo vyote vile vinavyoenda  kinyume na maadili katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo Mkoani hapa.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Arusha,Abel Mtopwa aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake na kuongeza kuwa jukumu hili sio la kuiachia serikali peke yake  kwani ni la jamii kwa ujumla.

“Ni jukumu la wazazi/walezi na waalimu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu nidhamu kwa wanafunzi na kuhakikisha kuwa wanakemea matendo
yote yale yanayoenda kinyume na maadili ya mtanzania kwawanafunzi”alisema

Mtopwa aliyasema hayo kufuatia hivi karibuni kuripotiwa taarifa ya baadhi ya wanafunzi kufundishwa vitendo vya kulawitiana  ambavyo ni kinyume na maadili katika baadhi ya shule zilizopo katika mkoa wa jirani wa Kilimanjaro.

Alisema kuwa Mkoa wa Arusha umechukua taadhari zote kukabiliana na matukio hayo na kwamba mpaka sasa hakuna shule hata moja iliyoripotiwa  kujihusisha na matukio hayo na kwamba wameishatoa maagizo kwa waalimu wakuu na maafisa elimu wa kata juu ya matukio hayo.

Afisa elimu huyo alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa kila mtoto amnayehitajika kwenda shule wahakikishe kuwa anaripoti kwani kwa sasa
hakuna kisingizio chochote ukizingatia kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya kujisomea pamoja na kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

“Nitoe wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanachangia kwa hiari chakula cha mchana kwa nanafunzi kwa mujibu wa waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2016 kwani jukumu la kumpa mtoto chakula,sare  na vifaa vyote
vya kujifunzia ni la mzazi”alisema.

Afisa elimu huyo wa Mkoa alisema kuwa mkoa wa Arusha ulitarajia wanafunzi elfu 4288 kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2023 na kwamba mpaka sasa wanafunzi elfu 3274 sawa na asilimia 75 wamekwishajiunga na kuwataka wale wote ambao hawajaripoti kuripoti shuleni mara moja.