Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amezindua kituo cha usambazaji wa mbegu kituo cha Shinyanga na kupokea shehena ya tani 100 za mbegu kutoka wakala wa mbegu bora nchini Agriculture Seed Agency (ASA)
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo Mh.Mjema amewataka maafisa kilimo wa ngazi zote kuwafikia wakulima na kuwaelimisha juu ya matumizi ya mbegu hizo hali ambayo itasaidia kuondoa umaskini.
Amekitaka chama cha ushirika mkoa wa Shinyanga Shirecu kutumia fursa hiyo kuleta mapinduzi ya kilimo yatakayoleta tija na ufanisi kwa mkulima na taifa kwa ujumla
“Lakini Shirecu nendeni kwa wakulima wenu sitaki tena nisikie shirecu mnalega lega hapa ndipo penye eneo la kuweza kuamka na kuweza kuwasaidia wakulima ili waondokane na umaskini nataka shirecu ilete mabadiliko katika mkoa huu”
Katika hotuba yake iliyohusisha uzalishaji na usambazaji wa mbegu unaofanywa na wakala wa mbegu bora nchini Agriculture Seed Agency (ASA) mkurugenzi mtendaji mkuu Dkt. Sophia Kashenge wameleta mbegu za mahidi na mbegu za alizeti ambapo amesema wataendelea kusambaza mbegu kadri ya mahitaji ya wakulima na wanunuzi.
“Kwa kuanzia tumeleta mbegu hizi kiasi cha tani laki moja na elfu tisa ambazo zinajumuisha kiasi cha mahindi tani elfu 89 na elfu 20 kwa ajili ya alizeti hii ni kwa uzinduzi tu tutasambaza mbegu kadri ya mahitaji ya wakulima na kuzileta hapa Shinyanga ni kama senta ya usambazaji ambazo zinaenda maeneo yote ya jirani na Shinyanga na kanda ya ziwa kwahiyo mtu yeyote atakaehitaji mbegu hizi atazipata”amesema Kashenga
Akizungumza katika hafla hiyo meneja mkuu wa Shirecu Jakson Nyanda ameahidi chama hicho kushirikiana na wakala wa mbegu bora Agriculture Seed Agency (ASA) ili kuhakikisha wakulima wa mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine wananufaika.
“Sisi shirecu tutashirikiana na ASA kwa nguvu zote ili kuhakikisha wakulima wote wanafanikiwa kama ndugu zetu wa ASA itawapendeza tukotayari kuwa na wakala wa kilimo ili tuwasaidie kusambaza hizi mbegu mpaka kijijini kwa wakulima wa kawaida”
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amesema atahakikisha wakulima walioko kijijini mbegu hizo wanazipata kwa bei ile ile ambapo amesema mbegu hizo atasimamia kuhakikisha zinatumika vizuri huku akiwaomba wakulima kuwa na utaratibu wa kutunza chakula kuacha tabia ya kuuza chakula chote watoto au familia ikabaki na njaa
Wakala huo umejipanga kusambaza mbegu kilo 163,692 za mbegu za alizeti aina ya standard seeds ambayo ni sawa na tani 163,693 na kwamba baada ya uzinduzi huo wakala utaendelea kusambaza kiasi cha mbegu kilichosalia katika mikoa husika kulingana na mahitaji ya kila mkoa.