Balozi wa angola amesifu rais samia

 Balozi wa Angola hapa nchini Sandro de Oliveira, amempongeza Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake aliosema ni wenye maono na wenye kuwajali Watanzania katika kufikia maendeleo ya kweli.


Balozi Sandro de Oliveira ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, mazu.gumzo ambayo yamefanyika Ofisi kwa Katibu Mkuu huyo, katika Makao Makuu ya CCM Dodoma, leo.


Amesema Rais Samia tangu ashike hatamu ya Uongozi amekuwa akionyesha umahiri na dhamira ya dhati ya kulifikisha taifa la Tanzania kwenye mafanikio ya kiuchumi na kijamii huku akionyesha pia kuwa na maono chanya kwa Taifa.


Katika ziara hiyo ya kukutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, Balozi Sandro de Oliveira aliambatana na mwakilishi wa Chama Tawala cha Angola MPLA Antonio Lobito.


Katibu Mkuu Chongolo na Balozi huyo katika mazungumzo yao walizungumza masuala mbalimbali ikiwemo yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Angola, kindugu, kidiplomasia na Uchumi.


Pia walizungumzia kuendelea kukuza mahusiano ya kindugu uliodumu kwa miaka mingi baina ya Vyama vya Ukombozi vya CCM na MPLA uliojengwa na waasisi wa Mataifa hayo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius  Nyerere na Hayati Agustino Netho.