Baraza la habari nchini kenya lavutiwa na klabu za waandishi wa habari tanzania

Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Arusha Claud Gwandu akimkabidhi zawadi ya fulani yenye nembo ya APC Kiongozi wa Baraza la Habari Nchini Kenya Victor Bwire
Viongozi na watendaji wa Baraza la Habari Nchini Kenya wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji wa klabu ya waandishi wa habari Arusha, nje ya ofisi za APC

 Na Mwandishi Wetu,  Arusha

Viongozi wa Baraza la Habari nchini Kenya wametembelea ofisi ya klabu ya Waandishi wa Habari Arusha (APC), leo Disemba12, 2022 na kuahidi kuanzisha ushirikiano na  klabu za waandishi wa habari nchini.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Kiongozi wa baraza hilo Victor Bwire amesema baada ya kupata maelezo ya namna klabu za waandishi wa habari Tanzania zinavyofanya kazi chini ya UTPC, Baraza lake litaanza mikakati ya kuanzisha klabu za waandishi wa habari nchini Kenya na ataitumia Tanzania kama mfano wa kuwezesha zoezi hilo.

” Sisi nchini Kenya hatuna klabu za Waandishi wa habari, lakini kwa mfano ambao tumeuona hapa kwenu, na sisi tukirudi tunaenda kuanza mchakato wa kuanzisha klabu za waandishi,” amesema.

Bwire amesema Baraza la habari nchini Kenya wameanzisha mtandao maalum kwaajili ya kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao unaojulikana kama Africa Media Academy, ambapo waandishi watapata fursa ya kusoma masomo mbalimbali  na watakapohitimu watapatiwa cheti.

Mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa habari Arusha (APC), Claud Gwandu amesema klabu za waandishi wa habari zimefanikiwa kuwaleta pamoja waandishi wa habari kupitia klabu za waandishi zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania.

Amesema kupitia umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), waandishi wamekuwa wakijiunga kwa hiyari katika klabu hizo na kuendesha mambo yote yanayohusu maslahi ya wanahabari ikiwemo kutetea maslahi yao pindi wanapopatwa na majanga tofauti.

Viongozi wa APC, Katibu Mkuu Mtendaji Zulfa Mfinanga, Mwenyekiti Claud Gwandu na viongozi wa baraza la habari nchini Kenya wakiwa wameshika nembo ya APC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *