Bodi ya tanapa yawatunza wagumu tzs mil5, ni waliobeba mizigo ya waliopanda kilele cha mlima kilimanjaro maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara akipokea zawadi ya maua kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kigaigai baada ya kupokea waliokuwa wameshuka Mlima Kilimanjaro ktk maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru

 Na Seif Mangwangi, Kilimanjaro

BODI ya wakurugenzi ya Mamlaka ya hifadhi za Taifa (TANAPA), imetoa zawadi ya Milioni5 kwa wapagazi maarufu kama ‘wagumu’ baada ya kufanikisha vyema zoezi la safari ya watanzania 150 waliopanda Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka60 ya Uhuru.

Mwenyekiti wa waongoza watalii  mlima Kilimanjaro, Faustine Chombo ambaye pia ndiye muongoza watalii Mkuu wa kampuni ya utalii ya Zara ambayo ndio iliyoshirikiana na TANAPA kupandisha wageni150 ktk sherehe za miaka 60 ya uhuru mwaka huu

Akitangaza kutoa zawadi hiyo wakati wa hafla fupi ya kupokea msafara huo ulioongozwa na Kanali Martin Msumari wa JWTZ, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Jenerali Mstaafu George Waitara amesema wagumu wamekuwa wakifanya kazi ngumu kuhakikisha mpanda mlima anafanikiwa kufika kilele cha uhuru.

” Kupanda Mlima Kilimanjaro ni kazi ngumu sana, wapagazi maarufu kama wagumu wamekuwa wakifanya kazi ngumu sana, liwake  jua, inyeshe mvua wao lazima wahakikishe mpanda Mlima amefika Kileleni, naomba tuwapongeze na kwa kuwa wamefanyakazi ngumu leo kupitia bodi yangu nawapa zawadi ya Milioni5,” alitangaza Waitara.

Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu 2021 amefurahishwa na wajumbe wawili wa bodi ya TANAPA waliojitokeza kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea mandhari nzuri ya Mlima huo, lakini pia menejimenti ya Tanapa litasaidia wakati wa kufanya maamuzi mbalimbali kuhusiana na uboreshaji wa Mlima huo.

Waitara pia amesema amepokea maoni ya wadau kuhusu wageni wanaopanda mlima Kilimanjaro  kupewa ngao (kidani),  mbali na cheti ili kulivaa wakati wote na kuonyesha alama ya kupanda mlima huo  hivyo amewaachia menejimenti ya TANAPA kutafakari hilo na kuona namna ya kulifanikisha.

Ameishukuru kampuni ya utalii ya Zara Tours Kwa kufanikisha zoezi la kupandisha wageni 150 katika Mlima Kilimanjaro na kusema pamoja na kwamba hiyo ni safari ya kwanza katika historia kuwa na wageni wengi lakini kampuni hiyo imeweza kufanikiwa.

” Wageni 150 sio jambo la mchezo kabisa lakini tumeshuhudia wafanyakazi wa kutosha kuanzia waongoza watalii(guides) na wapagazi (wagumu ) wa kutosha ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuhakikisha  wageni wote wanapanda Mlima bila kikwazo, niseme tu hongera sana kwa Zara ikiongozwa na Mama Zara kama ambavyo tumezoea kukuita,” alisema Waitara.

Kanali Msumari alikabidhiwa Bendera ya Taifa Disemba5, mwaka huu na Naibu Spika Tulia Ackson na kutakiwa kuongoza watanzania 150 na kuiweka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni kumbukizi ya miaka 60 ya Uhuru.

Baadhi ya watu waliopanda Mlima Kilimanjaro wakiwa njiani kurudi baada kukamilisha zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro ktk maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru

Msafara huo uliojumuisha watu kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wanajeshi, waandishi wa habari, watendaji katika taasisi za Serikali na binafsi ulianza safari Desemba 5,mwaka huu kwenye geti la Marangu majira ya saa saba mchana na wapandaji kukamilisha siku ya kwanza katika kituo cha Mandara.

Safari hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Uwakala wa Utalii ya ZARA siku ya pili wapandaji walitembea hadi katika kituo cha Horombo Hut na kukaa kwa siku mbili na siku ya nne walitembea hadi katika kituo cha Kibo Hut umbali wa Kilometa 11 kabla ya siku ya tano usiku wa saa5 kuamkia Disemba 9, 2021 kuanza kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro. 

Kwa upande wake kiongozi wa msafara huo Kanali Martin Msumari amesema hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA),Shirika la TANAPA na kampuni ya utalii ya Zara kwa pamoja zimeweza  kuandika historia kubwa  kwa mara ya kwanza wapandaji150 wamepanda mlima Kilimanjaro.

Amesema katika safari hiyo wapandaji mlima 79 walifanikiwa kufika kilele cha Uhuru ikiwa ni historia ya kwanza katika mlima huo kwa idadi kubwa sana kufika kilele hicho cha urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari.

Kanali Msumari amesema waliopanda hadi fkituo cha Stella kituo kimoja kabla ya kufika kilele cha Uhuru  walikuwa wapandaji 3, Gilmans point 5, na waliotembea hadi eneo la Kibo Hut walikuwa30, Horombo Hut 20 na Mandara Hut8.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye alikabidhiwa Bendera na Kanali Msumari, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kigaigai alisema Mlima Kilimanjaro unapaswa kulindwa kwa ushirikiano wa watu wote kwa kuwa ni hazina kubwa ya hifadhi ya uoto wa asili na maji yake yamekuwa chanzo kikubwa cha uhai wa wakazi wa kanda za kaskazini na Mashariki.<

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kigaigai akitoa hotuba yake mara baada ya kupokea waliopanda mlima Kilimanjaro ktk maadhimisho ya miaka60 ya uhuru

“Nilipofika hapa Kilimanjaro kaka Mkuu wa Mkoa nilitembelewa na Mhifadhi wa Kinnapa Angela, alinieleza mambo mengi kuhusu Mlima, tangu siku hiyo niliamua kuwa balozi wa mlima huu kwa kuwa ndio unaopeleka maji mto pangani na nyumba ya Mungu na kutumika kuzalishia umeme lakini pia shughuli za umwagiliaji huko chini wanatumia maji haya lakini pia matumizi ya kawaida maji yake yote yanatoka hapa,”Alisema Kigaigai.

Katika Mahojiano maalum na Mkurugenzi wa kampuni ya ZARA, Zainab Ansel alisema kuwa wakiwa kama moja ya waandaaji wa safari hiyo wametoa jumla ya watu 250 wakiwemo wabeba mizigo na wapishi 185 huku waongoza utalii wakiwa ni 62.