Na Mwandishi Wetu.
Benki ya CRDB imeshiriki katika Wiki ya Uvumbuzi kwa Mwaka huu 2021 , Mada kuu ya mwaka huu ni “Ubunifu kwa Uchumi wa Kidijitali Stahimilivu na Jumuishi ( Innovation for a Resilient and Inclusive Digital Economy ) ”. Wiki ya Ubunifu Tanzania imekua kwa kasi kutoka mwaka 2015 ikiwa na wahudhuriaji karibu 500 hadi mwaka jana, 2020 ilipoudhuriwa na zaidi ya watu takribani 7,000 na kuwa ya kitaifa zaidi. Wiki hii imetoa jukwaa kwa wabunifu wengi kuonekana, wadau zaidi kuunda ushirikiano wa maana, maarifa mengi ya kushirikishwa, mipango mingi ya ubunifu itakayoonyeshwa na masuala muhimu yanayohusiana na sera kujadiliwa.
Afisa Mkuu Uendeshaji wa Benki ya CRDB Bwana Bruce Mwile (Katikati) wakati wa mjadala uliolenga kuangalia mchango wa Teknolojia katika kuendeleza uchumi wa Kidigitali kulia na kushoto kwake ni wadau wa sekta na Taasisi nyingine.
CRDB Benki kama taasisi inayotoa huduma za kifedha imeshiriki katika mjadala uliolenga kuangalia mchango wa Teknolojia katika kuendeleza uchumi wa Kidigitali . Katika Mjadala huo Afisa Mkuu Uendeshaji wa Benki ya CRDB Bwana Bruce Mwile amesema Benki ya CRDB imetengeneza fursa nyingi kwa watumiaji wake na sasa inafanya jitihada za kushirikiana na watoa huduma za mitandao ya mawasiliano ya simu kuangalia namna bora ya kupunguza gharama kwa wateja .
“ukiangalia zipo fursa nyingi sana katika Benki yetu ya CRDB, katika Uvumbuzi tunaoufanya tunawajali watu wote hata wamachinga, walimu, watoto na hata sekta mbalimbali, na ukitaka kujua kwamba sisi ni Benki inayosikiliza wateja juzi tulizindua simu Banking na watu wakatoa maoni kwamba tupunguze makato na tulifanya ivyo” Alisema Bwana Bruce Mwile.
Afisa Mkuu Uendeshaji wa Benki ya CRDB Bwana Bruce Mwile akiongea na Waandishi wa Habari baada ya Mada kumalizika
Kwa upande mwingine Mkuu wa Kitengo cha Mabadiliko endelevu ya Biashara Benki ya CRDB Bi. Winfrida Wanyacha amesisitiza kuwa Benki ya CRDB iko kwenye mchakato kufanya ushirikiano na kampuni za simu ili waweze kushirikiana kwa pamoja kupunguza zile gharama ili kuweza kuwanufaisha Watanzania wa kawaida wanaotumia huduma za kibenki.
Maadhimisho ya Wiki hii ya Uvumbuzi 2021 (INNOVATION WEEK 2021) yanaendelea LAPF TOWER Makumbusho Jijini Dar Es Salaam.
Wadau wa Sekta na Taasisi mbalimbali walivyohudhuria na kushiriki katika mjadala wa leo