Dc mwilapwa -mazingira ndio uhai wa taifa, aipongeza tanga uwasa kwa kuweka juhudi kwenye utunzaji wa mazingira

 

MKUU wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa akieleza jambo kuhusu umuhimu wa wananchi kutunza mazingira wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi wa vyanzo vya maji zinazofanywa na
uwamakizi  wilayani Muheza kwa ufadhili wa Tanga Uwasa
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga
Uwasa Mhandisi Rashid Shaban akieleza jambo wakati wa ziara hiyo
Afisa
Miradi kutoka Tanga
Uwasa Ramadhani Nyambuka akizungumza jambo wakati wa ziara hiyo kulia ni
Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tanga
Uwasa Mhandisi Rashid Shabani katika aliyevaa ushingi ni Katibu Tawala
wa wilaya ya Tanga Faidha Salim

Afisa Miradi kutoka Tanga
Uwasa Ramadhani Nyambuka kushoto akieleza jambo wakati wa ziara hiyo

Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa kushoto akiwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Tanga Faidha Salimu  na Mwenyekiti wa kikundi cha
Uwamakizi,Twaha Rajabu wakitembelea maeneo ya uhifadhi wa mazingira

Afisa Miradi kutoka Tanga
Uwasa Ramadhani Nyambuka kushoto akieleza jambo wakati wa ziara hiyo

MKUU wa wilaya ya Tanga Thobias
Mwilapwa amesema mazingira ndio uhai wa Taifa na bila mazingira hakuna chochote
kinaweza kufanyika hivyo jamii haina budi kuhakikisha wanayatunza na kuyalinda
kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

DC Mwilapwa aliyasema hayo wakati
wa ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi wa vyanzo vya maji zinazofanywa na
uwamakizi Amani wilayani kwa ufadhili wa Tanga Uwasa ikiwa ni wiki ya mazingira ambapo vijiji
18 vipo katika utunzaji wa vyanzo vya Maji na Mazingira katika wilaya Muheza

Alisema kwa sababu bila mazingira
hakuna jambo lolote ambalo linaweza kufanyika hivyo ni muhimu kwa jamii
kuhakikisha wanaachana na vitendo vya kuharibu mazingira kwenye maeneo yao
badala yake washirikiane kuyalinda.

“Kwanza nipongeze ubunifu huu
uliofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) kwa
kushirikiana na jamii inayoishi kwenye vyanzo vya maji kuwapa elimu ya ya
utunzaji wa mazingira na hivyo kupelekea kuwa mabalozi wazuri katika kutunza
mazingira”Alisema

Mkuu huyo wa wilaya alisema jambo
kubwa ni jamii kubadilika katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanatunza mazingira
kila mtu aweze kunufaika na uwepo wake na Tanga Uwasa wamefanya jitihada za
kuondoa malalamiko ya Maji kutoka Muheza wanafaidika wengine kwani hivi sasa
kila kijiji kinafaidika na uwepo wa vyanzo vya maji hivyo ni muhimu kutunza
mazingira maji yapatikane kwa kila mtu na sasa vijiji vitatu vimeanza kupata
maji.

Alisema sehemu kubwa ya maisha ya
binadamu yanahitaji maji na asilimia 75 ya mwili wa binadamu ni maji na hata
kwenye vitabu vitakatifu vimeandikwa hata roho ya Mungu ilikua imetulia kwenye vilindi
vya maji kwa hiyo dhana ya maji ni kubwa katika uhai hivyo tuhakikisha
tunatunza mazingira yatupatie maji.

Awali akizungumza wakati wa  ziara hiyo ,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga
Uwasa Mhandisi Rashid Shaban amesema  katika wiki ya Mazingira wameamua kutembelea
jamii inayotunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kuendelea
kuhamamsisha umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji.

Alisema wao wafanya kazi za utoaji wa
huduma za maji katika wilaya ya Tanga, Muheza na Pangani lakini chanzo cha Maji
ni mto zigi ambao unaanzia kwenye milima ya Amani ambapo mito imeanzia hivyo
wakalazimika kwenda na Mkuu wa wilaya ya Tanga kumuonesha jitihada za Tanga
Uwasa ambazo wanazifanya katika vyanzo vya maji.

“Tunachokifanya ni kuwawezesha
wananchi wale wanaoishi kandokando ya vyanzo vya maji wafanye shughuli zingine
ambazo haziathiri uharibifu wa mazingira ambazo zinaathiri vyanzo vya maji na
hivyo kujiingizia kipato na kuendesha maisha yao”Alisema

Mhandisi Shabani alisema kupitia wadau
ambao ni wananchi waliopo vijijini shughuli zao nyingi zinahusisha kilimo,
kukata miti ambayo sio rafiki kwa mazingira wameona washirikiane nao
kuwawezesha kufanya shughuli zingine mbadala kuliko kufanya shughuli
zinazoathiri vyanzo vya maji.

Alisema madhara makubwa yanayotokana
na uharibifu wa mazingira ni pamoja na ardhi kuwa wazi na wa wale wanaolima
mvua zikinyesha zinabeba udongo hupelekwa mtoni na kusababisha udongo kujaa
kwenye bwawa na hivyo kusababisha gharama kubwa kwa mamlaka ili kununua dawa.

“Kwani uharibifu huo unapelekea
kazi ya kusafisha maji ni mwananchi ndio atakae umia kwa kuwa ni lazima bei ya
maji itapanda kwani tunasafisha maji kuondoa vumbi na kemikali itabidi Mamlaka
iingie gharama kununua dawa”Alisema

Hata hivyo Afisa Miradi kutoka Tanga
Uwasa Ramadhani Nyambuka alisema mambo wanayoyafanya katika uhifadhi wa ardhi
ni kuhakikisha tope haliendi mtoni kwa kutumia ubunifu wa kilimo cha matuta.

“Huku tunafanya kilimo cha matuta
kwa kutunza ardhi ambapo inapunguza kasi ya maji yanapotoka juu milimani kuzuia
kuepusha mmomonyoko na hivyo maji yanakuja taratibu yanafika sehemu yanatuama
yanaenda hatua nyingine inafanya udongo ujitenge na maji safi yanaenda
mtoni”Alisema Nyambuka.

Alisema
mradi huo wa utunzaji wa mazingira ulianza tokea mwaka 2013 ambapo elimu
ilianza katika vijiji vitano ambavyo vilikuwa na jumla ya wanachama 473 ambao
waliunda kikundi cha Uwamakizi

Alisema kati ya vijiji hivyo 18 ni
vijiji vitatu ndio vimeanza kupata huduma ya maji kwasasa ambavyo ni Kimbo,
Shembeleza na Mashewa.

Nyambuka alisema muungano huo haukuwa
rahisi kwa wananchi kuelewa Tanga Uwasa inahitaji nini katika utunzaji wa
mazingira lakini kadiri walivyokuwa wakitoa elimu kwa wananchi kila kijiji ili
kuelimisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira waalianza kueleza na kuanza kufanya
kilimo kisichoathiri vyanzo vya maji ili kuendelea kulinda vyanzo vya Maji.

“Katika kufanikisha malengo ya
utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya Maji,Tanga Uwasa tumefanikiwa kutumia
vikundi vya hamasa  kilianzishwa na
wananchi wenyewe wa kwa kuanzisha UWAMAKIZI na kuanza kuzunguka vijiji vyote
vyenye vyanzo vya maji na kuanza kutoa elimu,hamasa na mpaka sasa vijiji
vinavyojihusisha na utunzaji wa mazingira imefika 18 na vikiwa na wanachama
1540 “Alisema

Hata hivyo Mwenyekiti wa kikundi cha
Umakizi,Twaha Rajabu
amesema jamii inayozunguka
vyanzo vya maji walikua wanakawaida ya kufanya shughuli za kibinadamu ambazo
sio rafiki,ufanyaji kazi huo ulisababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji kuelekea
bwawa la Mabayani ambayo ndio inalisha Tanga mjini

“Hivyo kutokana na shughuli za
kibanadamu ambazo zilileta uharibifu,Mamlaka ya Maji Tanga Uwasa walianza na
sisi uwamakizi ili kuepusha  na kunusuru uharibifu wa  vyanzo vya
maji katika shughuli hizo tunatoa elimu kwa jamii kuacha kuchafua vyanzo vya
maji,na wapande mazao ambayo ni rafiki kwa vyanzo vya maji kuacha mita 5
zisiguswe kabisa na mita 55 kupanda miti ambayo inakua rafiki kwa mazingira
ambayo ni Kakao na Pilipili Manta” alisema Rajab