MAMLAKA ya udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imesema elimu mbali mbali ambayo wameendelea kutoa imefanikisha kupungua Kwa uuzaji mafuta holela kwenye vidumu maeneo ya Vijijini baada ya vituo vya mafuta kujengwa Vijijini .
Kaimu meneja wa EWURA kanda wa kati Mhandisi Martin Maurusi alisema hayo Leo wakati akitoa maelezo Kwa mbunge wa Makambako Deo Sanga aliyetembelea Banda la maonesho ya karibu kusini Katika viwanja vya Kihesa Kilolo mjini Iringa .
Alisema kuwa wao kama EWURA wanaendelea kujivunia mafanikio makubwa ya jinsi wanavyofikisha elimu kwa wananchi .
Aidha alisema kupitia elimu mbali mbali ambavyo wameendelea kutoa kumekuwepo na ongezeko kubwa la wananchi wenye uwezo wa kujenga vituo vya mafuta kujenga vituo katika maeneo ya miji na vijiji ili kuepuka kero ya wananchi kuuza mafuta kwenye vidumu .
Mbunge wa Makambako Deo Sanga akiwa na watumishi wa EWURA kwenye Banda la maonesho ya utalii ya karibu kusini
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Makambako mkoani Njombe Deo Sanga amepongeza jitihada kubwa za utoaji wa elimu mbali mbali ya maji na Nishati inayoendelea kufanywa na mamlaka ya uthibiti wa Nishati na maji (EWURA) chini ya mkurugenzi wake Mhandi Mosidestus Lumato kuwa zinakwenda sanjari na jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan .
Akizungumza baada ya kutembelea banda la EWURA katika maonesho ya utalii ya karibu kusini yanafanyika katika viwanja vya Kihesa Kilolo mjini Iringa , Mbunge Sanga alisema kuwa nguvu kubwa ya dunia na serikali ya Tanzania ni kuendelea kupambana na mabadiliko ya tabia Nchi kwa kuhimiza wananchi kutumia gesi na kuepuka matumizi ya kuni .
Alisema kuwa Rais Samia ameendelea kuhimiza matumizi ya gesi kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira hivyo elimu ambayo EWURA imeendelea kuitoa kwa wananchi juu ya matumizi ya gesi itasaidia zaidi kupunguza matumizi ya kuni na wananchi kugeukia matumizi ya gesi kwa ajili ya kupikia .
” Elimu hii nzuri ambayo EWURA mmeendelea kuitoa kupitia maonesho hayo ya utalii ya karibu kusini inapaswa kuendelea kuungwa mkono na kusambaa zaidi ili wananchi somo ya uhifadhi wa mazingira liweze kuwaingia zaidi ila niwapongeze sana tena sana kwa jinsi mlivyojipanga kuunga mkono jitihada za mheshimiwa Rais Samia katika utoaji wa elimu ya matumizi ya Gesi “
Aidha mbunge huyo alipongeza ukuaji wa Teknolojia nchini kwa kuwepo kwa magari yanayotumia gesi na kuwa iwapo hamasa itakuwa kubwa zaidi na vituo vya uuzaji wa gesi zitajengwa kila mkoa ni wazi watu wengi watageukia kununua magari yanayotumia gesi .
Mbunge Sanga alisema suala la elimu ya utalii kwa wananchi ni vema ikaendelea kufanyika sanjari na utunzaji wa mazingira maana kama matumizi ya kuni yatakuwa juu ni wazi utalii utakwama na kuwa hjitiada za Rais Samia kutangaza utalii ni kubwa zaidi na hivyo lazima utunzaji wa mazingira ukapewa nafasi .
Pia alishauri EWURA kuendelea kutumia vyombo vya habari kutoa elimu zaidi kwa umma juu ya matumizi sahihi ya gesi ili kuepuka uharibifu wa mazingira .
Awali akitoa maelezo kwa mbunge huyo afisa uhusiano wa EWURA Tobietha Makafu alisema kuwa mbali ya elimu mbali mbali ambazo EWURA imeendelea kutoa pia wameendelea kutoa elimu kwa mananchi kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni gesi .
Pia elimu ya matumizi ya mtungi wa gesi na kutambua ujazo sahihi wa gesi pamoja na kuchukua tahadhari ya matumizi sahihi ya gesi hasa baada ya kutoka kununua mtungi wa gesi ni lazima kwa mtumiaji kuacha kwanza mtungi huo kutulia kwa muda kabala ya kuanza kuutumia pia kuepuka kuwasha taa ama matumizi ya simu wakati wa kutumia mtungi wa gesi .
Akizungumzia matumizi ya gesi asilia kwenye magari alisema ni njia sahihi zaidi kutokana na gesi kupatikana hapa nchini tofauti na mafuta ambayo hutoka nje na kuwa tayari kasi ya wananchi kutaka kufungua vituo vya kuuza gesi asilia imeanza kuongezeka hasa kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani .
Huku kwa upande wake afisa mwandamizi wa huduma kwa wateja wa EWURA Muhiba Chakupewa alisema wao kama EWURA wameendelea kufikisha elimu ya gesi kwa wananchi mbali mbali mijini na vijijini .
Hata hivyo alisema kuhusu namna walivyojipanga kutoa elimu kuwa wamekuwa na vipindi mbali mbali vya elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari pia kupitia kitengo cha mahusiano cha EWURA wamekuwa wakitoa elimu mbali mbali hadi kwenye vikao mbali mbali vikiwemo vya vijiji.