Hatimaye mwili wa hayati lowassa wawasili nyumbani kwake monduli

Na Egdia Vedasto, Arusha

Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Nne Hayati Edward Ngoyai Lowassa umewasili Leo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuelekea nyumbani kwake katika Kijiji Cha Ngarashi wilaya ya Monduli mkoani Arusha. 

Wananchi wamepata nafasi ya kuaga mwili wa kiongozi huyo kwa kusimama pembezoni mwa Barabara  kuu ya kutoka uwanja wa ndege hadi wilayani Monduli ambapo wametoa heshima zao za mwisho kwa kupunga mikono huku shughuli zao zikisimama na wanafunzi kusimamisha masomo Yao kwa muda.

“Tutamkumbuka kwa mengi aliyotufanyia kiongozi wetu ikiwa ni pamoja kuanzisha shule za kata,  ambazo zimekuwa mkombozi wa wananchi kwani watoto wengi wamepata elimu na kufanikiwa kutokana na shule hizo,” amesema Jason Massunga”

Hayati Lowassa atakumbukwa kwa uanzilishi wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) ambacho kinazalisha wasomi na wataalam wa kutosha kutoka katika vitivo mbalimbali.

Kwa upande wa mmoja wa viongozi wa mila ya kimasai  kundi la Legwanani kutoka wilaya ya Simanjiro Jackson Teteyo amesema watamkumbuka Lowassa kwa ushirikiano wake mkubwa kwao ikiwemo kuwapeleka nchi za jirani Kenya na Uganda ili kupata elimu ya ufugaji bora ambao umeendelea kuwapatia faida kubwa.

Amesema katika kumuenzi kabila la wamasai wilaya ya Monduli tumetoa ng’ombe zaidi ya tisini huku ng’ombe wengine zipatazo mia tayari zimechinjwa kama kitoweo kwa waombolezaji.

Aidha wananchi katika Kijiji alichokuwa akiishi Cha Ngarashi  wameonyesha simanzi kubwa kuondoka kwa kiongozi huyo wakitaja mchango mkubwa wa maendeleo aliouonyesha katika jamii Yao.

“Alijitahidi sana kuhakikisha tunapata maji, umeme, vituo vya afya na Barabara za lami na ametimiza aliyokuwa ametuahidi tunamuombea kwa Mungu apumzike salama “amesema mwenyeji wa Ngarashi  Samson Laizer”

Hayati Lowassa alifariki tarehe 10 February na anatarajiwa kuzikwa tarehe 17 February mwaka huu nyumbani kwake katika Kijiji Cha Ngarashi wilayani Monduli.