Hospitali ya kam yaomba isaidiwe na serikali

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KAM ya Kimara Korogwe,jijini Dar es Salaam, Dk. Kandore Musika (kulia) akiwaeleza wageni mbalimbali waliotembelea hospitali hiyo huduma mbalimbali zinazopatikana hospitalini hapo katika siku ya kutambulisha hospitali hiyo kwa wadau (PICHA: MPIGA PICHA WETU)
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KAM ya Kimara Korogwe,jijini Dar es Salaam, Dk. Kandore Musika akiwaeleza wageni kuhusu vifaa vya mabara vya hospitali hiyo waliotembelea hospitali hiyo Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KAM ya Kimara Korogwe,jijini Dar es Salaam, Dk. Kandore Musika akiwaeleza wageni kuhusu vifaa vya mabara vya hospitali hiyo waliotembelea hospitali hiyo Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

 

Na Mwandishi Wetu

HOSPITALI ya KAM Musika imeiomba serikali iwape ushirikiano wa kutosha wawekezaji wazalendo waliowekeza kwenye sekta ya afya ili wawe endelevu kwaajili ya vizazi vijavyo.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Kandore Musika wakati wa ziara ya kutambulisha hospitali hiyo mwishoni mwa wiki Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam.

Dk. Kandore  ni mwanzilishi wa KAM Dar es Salaam Pharmacy Limited, kampuni inayoendesha huduma za afya ikiwa na zahanati, hospitali, maduka ya dawa na Chuo cha Tiba cha KAM College of Health.

Dk. Kandore alisema wadau wengi walitaka kujua mambo mbalimbali kuhusu hospitali hiyo hivyo aliamua kuwatengea siku hiyo kwahili ya kujionea yanayofanyika kwenye hospitali hiyo ambayo ilifunguliwa miezi miwili iliyopita.

Alisema watanzania waliowekeza kwenye sekta ya afya wanamoyo wa kusaidia wenzao kwani wawekezaji wengi kutoka nje wamewekeza kwenye miradi yenye faida na hawapendelei kuwekeza kwenye sekta ya afya.

Alisema yeye kama mtanzania mzalendo atashukuru kama atapata msaada wa serikali kila inapopata fedha kutoka mataifa mbalimbali kwaajili ya kusaidia maendeleo ya sekta ya afya.

Alisema misaada hiyo isielekezwe kwenye taaissi za serikali pekee kwani hata hospitali binafsi zinawahudumia mamilioni ya watanzania wanapokuwa na matatizo.

“Hii ni taasisi ya familia na taasisi ya familia kwa Tanzania haiwezi kudumu miaka mingi hivyo serikali isipoangalia hii taasisi inaweza kupotea hivyo wakipata fungu kutoka kwa wafadhili watufikirie sisi wazalendo tuliowekeza kwenye sekta afya,” alisema

Dk. Musika alisema lazima kuwe na ushirikiano wa thabiti baina ya sekta ya umma na binafsi  ‘Public Private Partnership (PPP) kwani wote wanajenga nyumba moja lakini kwa sasa hakuna ukaribu wa serikali kwenye kuwasaidia watu binafsi waliowekeza kwenye sekta ya afya.

“Hii ni taasisi kubwa ila hatuna uhakika baada ya miaka 20 kama KAM itabaki kuwa KAM ya leo hivyo serikali isipotuangalia inaweza isiwepo na isipokuwepo wananchi watapata shida sana, serikali iangalie hata namna ya kuingia ubia kwa kutuletea madaktari na mashine za vipomo mbalimbali, semina na kutunganisha na wadau wa nje,” alisema .

Alisema hospitali hiyo iko kwenye ngazi ya wilaya ikiwa na vitanda 122 na kuongeza kuwa kwa uhalisia ilipaswa kuanza kama hospitali ya Mkoa ila waliona ianze kwa ngazi ya Wilaya na baada ya muda wataibadili iwe ya Mkoa.

Alisema hospitali hiyo inavipimo vya aina mbalimbali na kwamba wamepanga kuifanya iwe ya vipimo kwa kuhakikisha vipimo mbalimbali vinapatikana hospitalini hapo.

 “Sisi hatuzingatii faida kwenye utoaji wa huduma zetu, tunatoa huduma kwa jamiii na lengo la hii hospitali ni kutoa huduma pia kwa wanafunzi wanaosoma hapa leo tunapanua wigo kushiriana na wadau mbalimbali na itafuata miongozo yote ya wizara ya afya,” alisema .

 

 

 

3. Wageni mbalimbali waliotembelea hospitali ya KAM Musika ya Kimara Korogwe wakipata maelezo kuhusu hospitali hiyo walipofika mwishoni mwa wiki kwaajili ya kujionea huduma zinazotolewa hospitalini hapo