Idara ya afya mkoa wa arusha waandaa mkakati kushirikisha waandishi kukabiliana na ebola na corona

Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Arusha Dkt Robert Hongo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mdahalo kuhusu magonjwa ya mlipuko
Mtoa mada kuhusiana na matokeo changa na hasi yaliyotoka na chanjo ya Uviko-19 katika maeneo ya Wamasai, Kulwa Mayombi akiwasilisha mada yake
Katibu Mkuu wa APC Zulfa Mfinanga akizungumza wakati wa kufunga mdahalo kuhusu magonjwa ya mlipuko. Zulfa pia aliwasilisha mada kuhusu athari zilizotokana na kuripoti kwa taarifa za ugonjwa wakati wa ugonjwa wa uviko-19

 Na Mwandishi Wetu, Arusha 

Idara ya afya Mkoa wa Arusha imesema inaandaa mpango mkakati wa ushirikiano  na tasnia ya habari Mkoani humo kwa lengo la kudhibiti tishio la magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa waandishi wa habari kuhusu  maendeleo ya ugonjwa wa uviko19, chanjo na tishio la ugonjwa wa Ebola, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt Robert Hongo amesema kufuatia kuwepo na tishio la mlipuko wa virusi vya Ebola Serikali imeanza mikakati ya kukabiliana nao.

Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu stahili kuhusu mlipuko wa magonjwa ka hayo ili waandishi waweze kuandika habari sahihi kwa umma.

” Waandishi ni watu muhimu sana katika idara yetu ya afya, juzi tulikuwa na kikao na mkuu wa mkoa kuhusu tishio la ugonjwa wa Ebola ambao tayari uko Nchini Uganda, Mkuu wa Mkoa ametuagiza tuanze kampeni ya kukabiliana na virusi hivi na waandishi ni moja ya makundi ambayo tutakutana nayo ili wapate elimu ya kutosha,”Amesema.

Amesema endapo mwandishi wa habari hatopata elimu sahihi kuhusu virusi vya ugonjwa huo ni rahisi wananchi kupata taarifa potofu na matokeo yake ni kuongeza hofu na woga miongoni wa jamii hali inayoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo.

Dkt Hongo ambaye pia ni mratibu wa magonjwa ya Mlipuko Mkoa wa Arusha amesema vifo vingi vilivyotokana na  mlipuko wa virusi vya uviko-19 vilisababishwa na hofu iliyosababishwa na taarifa potofu zilizokuwa zikitolewa na watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema idara ya afya Mkoa wa Arusha tayari imetenga vituo vya kupokelea wagonjwa watakaogundulika kubwa na maambukizo ya virusi ya Ebola na kwamba kwa kuanzia maeneo yote hatarishi ikiwemo mipakani na viwanja vya ndege wataalam wamewekwa.

kwa upande wake  Mratibu wa chanjo ya Uviko-19 Mkoa wa Arusha Dkt Wilson Boniphace amesema dalili zinaonyesha virusi vya Corona bado vipo Nchini na hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kuchanja.

Amesema takwimu za watu kuchanja kinga ya virus vya ugonjwa wa  uviko-19 imeendelea kuongezeka baada ya watu kugundua kutokuwepo kwa madhara yanayotokana na chanjo kama ilivyokuwa ikienezwa kupitia mitandao ya kijamii.

Dkt Boniphace amesema virusi vya ugonjwa wa Ebola ni vigumu kugundua mapema kwa kuwa dalili zake zinafanana na magonjwa kama ya malaria, ikiwemo mgonjwa kupata homa kali, kichwa kuuma na kutapika.

” Ugonjwa huu ni hatari sana, tangu umeingia Uganda umeshaua watu zaidi ya 60 na miongoni mwao ni madaktari kwa hiyo tunapaswa kuchukua tahadhari ya hali ya juu kudhibiti usiingie nchini na tunafanya hivyo  kwa kuwa sisi na Uganda ni majirani sana,”amesema.

Mdahalo huo umeandaliwa na Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na shirika la  Internews.