Jamii yaaswa kuwatunza wazee badala ya kuiachia serikali

Na Joachim Nyambo,Mbeya.
JAMII nchini imetakiwa kutambua kuwa jukumu la kuwawekea mazingira mazuri ya kimaisha wazee  ni la kila mmoja badala ya kuiachia Serikali pekee kutekeleza jukumu hilo.
Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya,Dkt Osimunda Mwanyika alibainisha hayo alipofungua Mkutano wa viongozi,wadau na wazee uliolenga kuingiza masuala ya wazee katika Mipango ya Serikali uliofanyika jijini Mbeya.
Dkt Osimunda alisema kumekuwa na dhana ndani ya jamii ya kuilaumu na kuitaka Serikali kutekeleza mambo mbalimbali kwa wazee lakini baadhi ya watu wanajisahau kuwa jukumu hilo linapaswa kuwa la pamoja kati ya Serikali na wadau mbalimba ikiwemo jamii inayowazunguka wazee.
Alisema ni wakati sasa kwa wadau wote kuungana kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wazee nchini ili kuwawezesha kuishi maisha ya furaha na yenye kuwafanya kufarijika kwa kuishi na jamii inayowajali.
Alizitaja taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini kuwa na umuhimu mkubwa katika kuibua na kuhimiza jamii kuwa na mikakati ya kuwasaidia wazee ikiwemo kuhimiza uwepo wa mifuko ya wazee.
“Ni muhimu tukaungana kuainisha changamoto zote zinazowakabili wazee.Taasisi mbalimbali ziwe za Serikali au binafsi na hasa za kidini zijikite katika kuwatetea wazee.Zihimize kuwepo kwa mifuko ya wazee.Ifike wakati sote tuseme ni lazima tutenge bajeti kwaajili ya wazee katika ngazi mbalimbali.” Alisisitiza Dkt Osimunda.
Aidha Dkt Osimunda alipongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali nchini,ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa matibabu hatua aliyosema imeleta unafuu hasa baada ya kutenga madirisha maalumu ya wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa upande wao wazee waliohudhuria mkutano wao kupitia taarifa yao iliyosomwa na mwenzao Hezron Kapwela waliitaka jamii kuzingatia Agenda za wazee 2020 zilizojadiliwa Februari mwaka huu jijini Dodoma katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Miongoni mwa agenda hizo ni pamoja na Kukamilisha uundaji wa mabaraza ya wazee katika ngazi zote nchini,Sera ya wazee kufanyiwa marekebisho na kutungiwa sheria,kuwa na uwakilishi wa wazee katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote na upatikanaji wa pensheni jamii kwa wazee wote walio na umria wa kuanzia miaka 60.
Nyingine ni kukomesha vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee,uwezeshaji kiuchumi na kipato kwa wazee,Huduma za Afya na matibabu bure kwao hasa kwa magonjwa yanayowasumbua zaidi watu wa umri wao pamoja na Taasisi za umma kuweka miundombinu rafiki na huduma nyinginezo za jamii kwa wazee.
Awali akizungumzia malengo ya Mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika na Kiuwauta lililoandaa mkutano,Amina Mwinami alisema bado kuna kusuasua kwa kuundwa kwa Mabaraza ya wazee katika ngazi mbalimbali hatua inayosababisha wazee kuendelea kukosa nguvu ya pamoja ya kujinasua kwenye changamoto zinazowakabili.