Maria Okama, afisa ustawi wa jamii, Manispaa ya Shinyanga |
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Serikali na wadau wengine Mkoani Shinyanga wametakiwa kutumia maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kutafakari kuhusu baadhi ya familia zinazotelekeza Wazee wao, kwani hali hiyo imetajwa kuwa ni tishio la usalama wa kundi hilo.
Kwa nyakati tofauti wakazi wa mji wa Shinyanga wamesema wakati serikali na wadau wakiendelea na mapambano ya kupinga ukatili wa aina nyingine,hali ya Wazee kutelekezwa na Watoto,ndugu au jamaa zao wa karibu imeendelea kushamiri na hivyo kusababisha kuwa na wimbi la wazee wanaohangaika mitaani na wengine kulelewa kwenye kambi maalumu za serikali.
Wamesema kupitia maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia serikali na wadau wengine wanapaswa kulichukua tatizo hilo kama changamoto nyingine ya kushughulikia.
Akizungumzia kuhusu hali hiyo Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga Maria Okama amesema familia zinazowatelekeza Wazee zinakwenda kinyume na maadili ya kijamii,na kwamba kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki za Wazee hao ambao wanakosa upendo na huduma za Msingi kutoka katika familia zao.
“Kwa sababu utandawazi umetawala kwenye akili za watoto akili zao zote wamezielekeza kwenye mambo ya kidunia kwahiyo wanasahau kuendelea kuyaisha yale maadili ya wazazi nawaasa wazazi waendelee kuwalea na kuwasimamia watoto wetu wakue katika maadili mazuri wasiache utamaduni wa asili wakaenda kuiga tamaduni za watu kwa hali hiyo na kwa kufanya hivyo itasaidia pia hata mtoto anapofanikiwa kuweza kukumbuka alikotoka na kuwaangalia wale waliomsaidia na kumfikisha pale alipofika lakini pia kuwa na hofu ya Mungu”.
“Ushauri wangu kwa watoto ambao wamewasahau wazazi wao warudi hata kama wameshakosea wajue kabisa wale ni wazazi wao ndiyo waliowalea na kuwasomesha mpaka kufika hapo walipo mafanikio waliyonayo ni kutokana na wazazi walionao wazazi wasinge simama kwenye nafasi yao kwa kuwahudumia na kuwasimama lakini pia kuwaelimisha wasingefanikiwa kwahiyo watambue kwamba nyuma yake kuna mtu aliye muwezesha yeye kufika hapo alipofika lakini pia wafundishwe maadili mema na kumuogopa Mungu ili kupitia hali hiyo waweze kutambua wao ni nani katika jamii”.
Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yamelenga kutoa nafasi kwa Serikali na wadau wake, kutathimini hatua za mafanikio zilizofikiwa katika mapambano lakini pia changamoto zilizojitokeza ili kuweka mipango na mikakati ya pamoja ya namna bora ya kukabiliana nazo.