Jiji la arusha kutoa mikopo ya mil400 kwa vijana, wanawake na walemavu

Viongozi wa vikundi 59 wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi wakati wa kufungua mafunzo hayo
Wawezeshaji wa mafunzo kwa vikundi vinavyopewa mkopo maafisa maendeleo ya jamii wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt Onesmo Mandike wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele
Viongozi wa vikundi vya walemavu wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha
Wawakilishi wa vikundi vya wanawake na Vijana wakiwa katika picha ya pamoja na kaimu mkurugenzi wa Jiji la Arusha

 Na Seif Mangwangi, Arusha 

Jiji la Arusha linatarajia kutoa mikopo isiyokuwa na masharti yoyote kwa  vikundi 59 vya wanawake, vijana na walemavu ikiwa ni robo ya pili ya mwaka wa  fedha ulioanzia Juni 2021.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Jiji la Arusha, Dkt Onesmo Mandike,  zaidi ya Shilingi Milioni 400 zinatarajiwa kutolewa ikiwa na lengo la kuwawezesha na kuwanyanyua kiuchumi wanawake,vijana na walemavu.

Akifungua mafunzo kwa viongozi wa makundi hayo matatu  yaliyoshirikisha  Mwenyeki, Katibu na  Mweka hazina, Kaimu Mkurugenzi Dkt. Mandike amesema fedha ambazo wanaenda kukopeshwa wananchi hao wa Jiji la Arusha zinatokana na sehemu ya mapato ya ndani ya Jiji.

Amewataka viongozi wa vikundi hivyo kusimamia  vizuri fedha watakazopewa na kuzirejesha kwa utaratibu watakaopewa ili ziweze kusaidia makundi mengine ambayo bado hayajapata.

“Leo mmekutanishwa hapa kwaajili ya mafunzo, naombeni mzingatie sana kile mtakachofundishwa, lengo kuu ni kuwawezesha kiuchumi, kwa hiyo lazima muwe na nidhamu ya pesa ili ziwapatie faida na mrejesho kama mtakavyopewa,” amesema.

Amewataka watakao kopeshwa fedha hizo kuzirejesha kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria na kwamba kuchelewesha marejesho ni kuyakosesha makundi mengine kupata mkopo kwa wakati.

Afisa uwezeshaji idara ya maendeleo ya jamii  Jiji la Arusha, Loishooki  Najun amesema fedha hizo zitagawanywa kwa mfumo wa asilimia 4,4,2 ambapo vikundi vya wanawake vitapewa Milioni 164, vijana Milioni 164 na walemavu Milioni 82.

“Vikundi 59nvinavyopewa mkopo ni kwa mgawanyiko wa vikundi 32 wanawake, vijana vikundi 16 na walemavu vikundi 11, mafunzo haya yanahusu nyanja zote za kiuchumi,”amesema.

Ametaja nyanja hizo kuwa ni pamoja na utafutaji masoko, ufugaji bora, ujasiriamali, namna ya kutunza kumbukumbu za uhasibu, lakini pia mafunzo ya afya hususani ugonjwa wa Ukimwi lengo likiwa ni kuwasadia kuepuka kutumia fedha hizo kwenye matumizi ya anasa na kupata maradhi ambukizi.

Loishooki  amesema Novemba mwaka jana 2021 jiji lilushatoa zaidi ya Mikopo ya Milioni 900 kwa makundi kama hayo ambapo  jumla ya vikundi 104  vya wanawake walipewa mkopo, vijana vikundi 36 na walemavu vikundi 8. 

Kwa upande wake Mratibu wa Vikundi vya kijamii Jiji la Arusha na msimamizi mkuu wa mafunzo kwa vikundi, Fatma Amir amesema vikundi vilivyochaguliwa vimekidhi vigezo vyote na kwamba kutokana na vigezo hivyo urejeshaji wa mikopo hautasumbua kama ilivyokuwa hapo nyuma.

Akitoa shukrani kwa mgeni rasmi Yunis Urasa ambaye ni mwenyekiti wa Shirikisho la walemavu Arusha (Shivyawata), amewataka wanavikundi wenzake kutumia vizuri pesa ya mkopo watakayopewa na kuirejesha kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa.