Joto lapanda maandamano chadema kesho jijini arusha

Mwenyekiti wa taasisi ya Sauti ya Watanzania, Dkt. Wilbroad Slaa

Egidia Vedasto

Arusha

Maandamano ya amani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yamekamilika kwa asilimia kwa 99 yanayotarajia kufanyika kesho asubuhi Jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo jijini humo Naibu Katibu Mkuu CHADEMA zanzibar  Salum Mwalimu amesema taratibu zimekamilika na kilichobaki ni kesho kuandamana.

” Ninachoweza kusema maandamano kwa siku ya kesho yapo,  tumejiandaa na tunaomba uzima ili tuweze kutimiza Lengo letu kama ambavyo tumejiandaa kwa muda mrefu na kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe tarehe13 Jan mwaka huu” amesema Naibu Katibu Mkuu Mwalimu

Naibu Katibu Mkuu, Salim Mwalimu akisisitiza madamano mbele ya Waadishi wa habari 

Mwalimu ameeleza kuwa kundi kubwa kutoka manyara, kutoka umasaini na wafanyabiashara wa biashara  ndogondogo wamejiandikisha kushiriki maandamano hayo yatakayoanza majira ya saa mbili asubuhi katika vituo vya Ofisi ya Hifadhi za Taifa (TANAPA),  kituo Cha Morombo na kwa mrefu, yatakayohitimishwa kwa kukutana katika viwanja vya reli.

Aidha ametaja viongozi kutoka sehemu mbalimbali watakaoshiriki kwenye maandamano hayo ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Tundu Lisu, Msigwa, Lema, Kiwangwa, Heche, Sugu pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Sauti ya Watanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa asasi hiyo Willbrod Slaa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sauti ya Watanzania Willbrod Slaa amewasihi Watanzania wa Kanda ya Kaskazini kujitokeza kuandamana ili kudai haki ya katiba mpya na kupinga yale mabaya yanayowaumiza wananchi wa hali ya chini.

” Mimi ni Mzee lakini ntawahi saa mbili Barabarani, nawasihi vijana amkeni tudai haki yetu ya katiba mpya  na Demokrasia huru takayotuletea mabadiliko ya Sheria kandamizi na zinazonyonya haki zetu Watanzania” amesema Slaa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha.

Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza katika kikao hicho na Waandishi wa Habari akisisitiza madamano ya kesho

Wakili kutoka Sauti ya Watanzania Boniface Mwabukusi ameeleza kwamba maandamano ni hatua za kutuma ujumbe kwamba  kinachofanywa na serikali hakikubaliki na kwamba Watanzania wamechoka na hawako tayari kuvumilia.

“Fursa kama bandari tumepata kwa mapenzi ya Mungu lakini utashangaa wanapewa wageni kwa mikataba haramu.  hiyo ni  mali ya Watanzania hivyo tuko tayari kupambana ili kuokoa rasilimali zingine, lakini pia niikumbushe serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika katika uchaguzi wa mwaka 2020 kisijirudie kwani hatutakubali na tumejipanga katika uchaguzi wa mwaka 2025 hivyo tunategemea kuona haki ikitendeka” Amefafanua Wakili Mwabukusi .

“Nawambia ndugu zangu wananchi mthubutu na  msiogope kuandamana  kwani Hali ya Watanzania wengi ni mbaya na hii ndio fursa pekee ya kuionyesha serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea Watanzania Maendeleo na badala yake imekuwa kilio na kukosa matumaini ya badae” Mwabukusi amesema”