Kampuni 500 kushiriki maonyesho ya timexpo 2024 dar

Na Mwandishi
Wetu

Dar es salaam

SHIRIKISHO la
Wenye Viwanda nchini  ( CTI) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), wamezindua  mipango ya ushiriki wa Maonesho ya Kimataifa
ya Wazalishaji Tanzania 2024, Tanzania International Manufacturers Expo
(TIMEXPO2024).

Maonesho
hayo yamepangwa kufanyika kuanzia Februari 26 hadi 29 mwaka huu katika viwanja
vya Sabasaba Dar es Salaam ikiwa ni mara ya pili tangu CTI na Mamlaka ya
Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuingia makubaliano ya kufanya
maonesho hayo.

 Lenard
Tenga, ambaye ni Mkurugenzi wa (CTI), ameeleza matumaini yake kwa maonesho ya
mwaka huu, akisisitiza lengo lake la kukuza ushirikiano kati ya wazalishaji wa
ndani na wazalishaji wa kimataifa.

Akizungumzia
kauli mbiu ya “Kujenga Daraja na kukutanisha wazalishaji wa ndani na Nje,”
Tenga aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuinua uzalishaji wa ndani hadi
kuwa na viwango vya kimataifa.

 Fortunatus
Mhambe ambaye ni Mkurgenzi wa Kukuza Biashara TANTRADE, akimwakilisha
Mkurugenzi Mkuu wa (TANTRADE), alionesha umuhimu wa kuunganisha viwanda vya
ndani na vya nje na kueleza jukumu la tukio hilo katika kurahisisha
kubadilishana maarifa na maendeleo ya kiteknolojia, muhimu kwa kuweka viwanda
vya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Pia Mhambe
aliwahimiza wadau kushiriki kikamilifu, kwani zaidi ya makampuni 500 kutoka
masoko ya ndani na kimataifa yanatarajiwa kushiriki kwa kuonyesha bidhaa na
huduma zao.

Kwa upande
wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) linatazama maonesho haya kama
fursa muhimu kwa wajasiriamali na wabunifu wa ndani

Kaimu
Mkurugenzi Maendeleo ya Teknolojia na Viwanda ‘SIDO’ Mhandishi Kulumuna
Benedicto alithibitisha nia ya SIDO kuwawezesha wazalishaji wa Kitanzania, hasa
kwa kutoa njia za kujifunza na kufikia masoko ya nje.

Hata hivyo
Ushiriki wa SIDO katika maendeleo ya teknolojia mbalimbali unathibitisha
dhamira yao ya kukuza uzalishaji wa kitaifa na ukuaji wa kiuchumi.

Aidha Masoud
Kipanya, Mkurugenzi wa Kaypee Motors, alisisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo wa
uzalishaji wa ndani na kutilia mkazo hoja ya Tanzania kubadilika kutoka kuwa
wanunuzi wa bidhaa peke na kuanza kuwa wazalishaji zaidi, akiongeza kuwepo na
ushirikiano na washirika wa kimataifa ili kuimarisha ujuzi wa viwanda,
akisistiza zaidi katika umuhimu wa kutumia maarifa na rasilimali za nje kukuza
viwanda vya ndani.

Huku
Tanzania ikijiandaa kuandaa Maonyesho ya Kimataifa ya Wazalishaji 2024, hamu ni
kubwa kwa mkusanyiko unaotarajiwa kusukuma ubunifu, ushirikiano na ukuaji
katika tasnia ya viwanda nchini. Kwa wingi wa washiriki, mijadala yenye
mafanikio, na fursa za mtandao, tukio hilo limepangwa kuonyesha uwezo wa
Tanzania kama kitovu cha ubora wa kimataifa katika uzalishaji wa viwandani.