Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wanakikundi wa jukwaa la mtandao wa WHATSAPP linalojulikana kwa jina la “Together we Fight” la Mkoani Shinyanga leo wametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula, vifaa vya shule pamoja na nguo kwa wasichana wanaolelewa katika kituo cha Agape.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mchele kilo 300, unga kilo 200, maharage kilo 25, sukari kilo 25, chumvi,mafuta, nguo,taulo za kile, daftari, kalamu pamoja na chaki ambavyo thamani yake ni zaidi ya shilingi Milioni moja.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo kiongozi wa jukwaa hilo ambaye pia ni Afisa uchumi wa Manispaa ya Shinyanga Gwakisa Mwasyeba amewataka wanafunzi hao kuongeza juhudi katika masomo ikiwa ni pamoja na kuzingatia nidhamu pamoja na upendo.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo wasichana wanaolelewa katika kituo cha Agape wameshukuru na kusema kuwa msaada huo utachochea ari ya kujifunza na kufanya vizuri zaidi kitaaluma.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo cha Agape John Myola amewashukuru wanakikundi kwa kutoa msaada huo ambapo amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto zanazowakabili wanafunzi.
Lengo la wanakikundi hao kutoa msaada huo ni kutaka kujenga utamaduni wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya shughuli za kijamii badala ya kutumia majukwaa hayo kwa matumizi mabaya.
Jukwaa hilo linajumuisha wanachama 120 kutoka kwenye makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo watumishi wa umma, taasisi , makampuni, mashirika pamoja na wafanyabiashara.