Na Mwandishi Wetu, Njombe
Kaimu Mkuu wa Mkoa, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Kasongwa amewataka Maafisa Mifugo kutoa elimu ya kutosha kwa wafugaji ili kuweza kufanikisha zoezi la Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo kwenye Halmashauri zote za Mkoa huo.
Mhe. Kasongwa ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya uhamasishaji wa zoezi la Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo kwa Mkoa wa Njombe, Disemba 13, 2021.
Akiongea na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Maafisa Mifugo, Maafisa TEHAMA na Maafisa Utambuzi wa Halmashauri zote za Mkoa Njombe, alisema ili zoezi la utambuzi wa Mifugo liweze kufanikiwa vizuri ni vyema wafugaji wapate Elimu ya kujua faida za utambuzi wa Mifugo ikiwa ni pamoja na kupata uhakika wa soko la mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
“Hatuwezi kupata maendeleo kama tutakaa kama kisiwa, tunatakiwa kwenda kama nchi za wenzetu wanavyoenda”, alisema Mhe. Kissa Kasongwa.
Aliongeza kusema kuwa, mifugo ikitambuliwa itawezesha nchi kuuza mifugo na mazao yake katika masoko yenye faida ya nchi za nje na hivyo kutoa fursa kwa Sekta ya Mifugo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kipato cha mtu mmoja mmoja.
Aidha, Mhe. Kasongwa amesema ili wafugaji waweze kupata faida ni lazima wafuate taratibu za kimataifa na ni lazima kupata elimu ya kufikia viwango vya afya ya wanyama vinavyokubalika na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) ambalo limekasimiwa madaraka na Shirika la Biashara Duniani (WTO) ya kuweka viwango vya Usalama wa Afya ya Wanyama (SPS Agreements) kupitia biashara salama ya wanyama na mazao yake.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari amesema ni uamuzi mzuri wa Wizara iliyouchukua wa kutoa elimu kwanza kwa wadau wa Sekta ya Mifugo ili kuweza kuona umuhimu na faida za utambuzi wa mifugo yao kabla ya kuanza zoezi hilo.
Bi. Judica ameongezea kwa kusema katika zoezi hilo wataalamu wa Mifugo wanatakiwa kuwa na kitu cha motisha cha kuwavutia wafugaji kukubaliana na zoezi hili la Utambuzi na Usajili wa mifugo yao na kuona umuhimu wa kugharamia uvalishaji hereni kwa mifugo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Juma Sweda ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuishirikisha Mikoa na Halmshauri na kuona ni muhimu kwa Wakuu wa Wilaya na Wataalamu wote ngazi ya Halmashauri kupewa mafunzo ili kuwapelekea elimu wafugaji walioko kwenye maeneo yao.
Mhe. Sweda amewasihi walioshiriki mafunzo hayo ya Utambuzi na Usajili wa Mifugo waende kuyafanyia kazi mafunzo yote waliyoyapata kupitia wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.