Mahakama kuu kanda ya dar es salaam imetupilia mbali mapingamizi ya serikali kwenye kesi ya tundu lissuNa Karama Kenyunko, Jamii Blog

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali mapingamizi ya awali ya serikali na Septemba 2, 2019 itaanza kusikiliza rasmi maombi ya msingi ya Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,Tundu Lissu, ya kuomba kibali cha kufungua shauri kupinga kukoma kwa ubunge wake.

Mapema, upande wa serikali uliwasilisha hoja tisa za pingamizi za kutaka maombi hayo yasisikilizwe kwa sababu yanamapungufu kisheria na kuiomba mahakama iyatupilie mbali.
Hatua hiyo imekuja baada ya Jaji Sirillius Matupa kusoma uamuzi na kukubaliana na majibu ya hoja zilizotolewa na jopo la mawakili wa Lissu, linaloongozwa na wakili Peter Kibatala na kutupilia mbali mapingamizi hayo.
Jaji Matupa amesoma uamuzi huo baada ya kupitia na kuchambua hoja za Serikali za pingamizi hilo alilolisikiliza Ijumaa iliyopita na majibu na mawakili wa Tundu Lissu, dhidi pingamiizi hilo.
Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu, Masijala Kuu, Dar es Salaam chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.
Katika maombi hayo dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungau shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.
Maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa juzi Ijumaa Agosti 23, 2019, lakini yalikwama baada ya Serikali kupitia kwa AG, waliwasilisha pingamizi la awali akiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo bila hata kuyasikiliza.
Katika pingamizi hilo la awali, Serikali iliwasilisha jumla ya hoja tisa, ikipinga kusikilizwa kwa maombi hayo kwa madai kuwa yana kasoro za kisheria. 
Katika uamuzi wake le Jaji Matupa ametupilia mbali pingamizi la awali la Serikali isipokuwa hoja moja tu ya kasoro katika viapo vinavyounga mkono maombi ya Lissu.
Kutokana na kasoro hizo Jaji Matupa amesema inapotokea kuwa kuna aya zenye kasoro za kisheria namna pekee ni kuziondoa aya hizo katika kiapo hicho na kuangalia kama aya zinazobaki zinaweza kusimama na kuthibitisha maombi.
Hivyo hoja zote za pingamizi la Serikali zimekataliwa isipokuwa hizo zenye upungufu kwenye hati za viapo. Ukiachilia mbali kasoro hizo za viapo, mambo mengine yote yataasikilizwa wakati wa usikilizwaji wa maombi ya msingi.”
Jaji Matupa amesisitiza kuwa pingamizi haliweza kuondoa haki za msingi kuwasikiliza wadaa kama kuna hoja za msingi za kusikilizwa.
Kuhusu hoja ya kusitisha kwa muda kuapishwa kwa mbunge mteule wa Singida Mashariki, Faraji Mtaturu, Jaji Matupa amesema kuwa sasa ni mapema mno kulitolea uamuzi na kwamba atalisikiliza ombi hilo wakati wa usikilizwaji wa maombi ya msingi.
Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge Spika Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *