Mama asha aihasa jamii kuwathamini watoto yatima.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi amewakumbusha wanajamii kuelewa kwamba Watoto yatima wanastahiki kupendwa zaidi ndani ya Familia ili kuwapa moyo na nguvu za kuondokana na mawazo ya kufikiria kupoteza Wazazi wao waliotangulia mbele ya haki.

Mama Asha ametoa kumbusho hilo wakati wa Dua Maalum ya kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki ambayo ilihudhuriwa na Watoto yatima wa Wilaya ya Kaskazini  “B” iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi ya CCM Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Mahonda.
Dua hiyo iliyoambatana na Chakula cha Mchana imeandaliwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar { ZARDEFO} kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo na Elimu ya Hayrat Foundation kutoka Nchini Uturuki.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar {Zardefo} Sheikh Sleyum Jumbe amesema Taasisi ya Maendeleo ya Elimu na Jamii ya Nchini Uturuki imefanya kazi kubwa katika kuunga mkono Jumuiya yao kwenye masuala mbali mbali ya Kijamii.
Akitoa salamu katika Dua hiyo Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Jamii na Elimu ya Hayrat Foundation Sheikh Adnan amesema Sekta ya Elimu inayotiliwa mkazo na Taasisi yao hulenga  kutanua wigo  wa Elimu inayomfungulia Mwanaadamu mwanga wa mafanikio katika maisha yake ya Dunia  na milele.