Mamia wajitokeza kuaga miili waliopata ajali ngaramtoni

Waziri Pindi Chana akitoa heshima za mwisho kwa marehemu waliopata ajali jijini Arusha

Na Egidia Vedasto

Arusha

Wananchi wamejitokeza kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali iliyotokea tareha 24 February mwaka huu katika maeneo ya ngaramtoni jijini Arusha.

Viongozi mbalimbali wameungana na waombolezaji katika taratibu za kuaga miili ambapo ndugu na jamaa wamejitokeza kwa wingi ili kuendelea na taratibu za mazishi baada ya utaratibu huo kukamilika.

Akitoa salam za rambirambi Waziri wa katiba na sheria Pindi Chana amesema msiba huo ni mzito na unamgusa Kila mmoja aliyeko ndani ya nchi na nje ya nchi hivyo ushirikiano unatakiwa katika kukamilisha maombolezo haya.

“Ndugu zangu huu msiba ni wetu sote hatuna budi kuungana kwa pamoja na tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe marehemu wote na awapungizie adhabu ya kaburi” Waziri Chana ameeleza kwa masikitiko.

Mkuu wa Mkoa Arusha John Mongela akitoa salam za rambirambi kwa wananchi jijini Arusha

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongera amesema wananchi wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imepokea kwa masikitiko makubwa na anaendelea kutoa pole nyingi sana kwa wananchi wote walioguswa na msiba. 

“Huu msiba ni wetu sote na tunatambua kwamba Taifa limepoteza nguvu kazi kubwa ndio maana tumegharamia mahitaji yote ikiwemo usafirishaji wa miili kwa watakaozikwa ndani ya Mkoa wa Arusha na nje ya Mkoa huo” amesema Mongela.

Naibu Balozi kutoka ubalozi mdogo wa Kenya nchini Tanzania Nancy Sifa akitoa Salam za rambirambi katika viwanja vya Shekhe Amri Abeid jijini Arusha

Hivyo hivyo Naibu balozi ndogo kutoka Kenya nchini Tanzania Nancy Sifa amesema ni masikitiko makubwa kwa msiba huo kwa sababu Taifa la Tanzania na Mataifa mengine yamepoteza nguvu kazi katika ajali hiyo 

“Nchi yetu ya Kenya tumepoteza watu wetu kwahiyo tunaungana na nanyi katika maombolezo haya katika maombi na Sala juu ya ndugu zetu waliopoteza maisha na wale waliopoteza ndugu zao katika ajali hii mbaya” nimaneno ya Nancy akitoa salam za rambi rambi katika uwanja wa Shekhe Amri Abeid Leo jijini Arusha.

Ajali hiyo ilihusisha magari manne roli na magari madogo matatu ambapo watu 25 walipoteza maisha na wengine 21 kujeruhiwa, na inaelezwa majeruhi wameruhusiwa kurudi nyumbani huku watano wakiendelea na matibabu kati Yao wanne wakiwa ni raia wa kigeni na mmoja Mtanzania.