*mbunge mavunde akabidhi matofali 5000 ujenzi wa sekondari nkulabi dodoma jiji*

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amekabidhiwa matofali 5000 yenye thamani ya Tsh 8,000,000 kwa uongozi wa Kata ya Mpunguzi sambamba na saruji mifuko 100 kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Nkulabi.

Shule hii ya Nkulabi inajengwa na Mbunge Mavunde akishirikiana na wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kuwapunguzia mwendo wanafunzi wa sekondari wanaotembea mwendo wa kilomita zaidi ya 9 kufuata shule.

“Nawapongeza sana wananchi wa Nkulabi kwa moyo wenu wa kujitolea mpaka tumeifikisha wote hapa ujenzi wa Shule hii.,”alisema na kuongeza:

“Tunashukuru pia Jiji la Dodoma kwa kutenga fedha Tsh 40,000,000 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha madarasa haya matatu ambayo tumeyaanza. Pia tunampongeza Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa ahadi ya ujenzi wa madarasa 15,000 ambayo pia shule yetu hii itaguswa kwa namna moja au nyingine”Alisema Mavunde.

Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma,Naibu Mstahiki Meya wa Jiji, Emmanuel Chibago amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwahudumia wananchi na kuwakikishia kwamba Jiji la Dodoma litaendelea kutenga fedha   kuboresha miundombinu ya Elimu na kuunga mkono juhudi za wadau kama Mbunge Mavunde pamoja na ninyi wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Nkulabi Diwani wa Kata ya Nkulabi, Innocent Nyambuya amempongeza Mbunge Mavunde kwa namna anavyoshirikiana nao kutatua changamoto mbalimbali za kwenye sekta ya Elimu na kuahidi kuwa nae bega kwa bega katika kuwaletea maendeleo wananchi.