Mhe. mtanda atoa onyo kali kwa wauza chuma chakavu.

Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Arusha

Na Zulfa Mfinanga,

Arusha.

Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda ametoa onyo kali kwa wanunuzi wa vyuma chakavu wanaohujumu nyara za serikali ikiwemo vyuma vinavyotumika kwenye Zoezi la anwani za makazi na kusema yeyote atakayekamatwa atashtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi.

Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo leo wakati akikagua vituo vya uuzaji wa vyuma chakavu vilivyopo mjini Arusha na kusema kuna baadhi ya wafanyabiashara wananunua na kuuza vyuma ambavyo vinavyotokana na miundombinu ya serikali ikiwemo vinavyotumika kwenye Zoezi la anwani za makazi.

Amesema kwa sasa Serikali ipo kwenye Zoezi la anwani za makazi hivyo ni vyema watu wenye nia ovu ya kununua au kuuza miundombinu ya Serikali kujiepusha na vitendo hivyo kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi hivyo haitavumilia kuona mali zake zikihujumiwa.

“Tutaita kikao na wauza vyuma chakavu wote Ili niwaambie haya, na endapo tutakukuta na chuma chakavu kinachotokana na miundombinu ya Serikali mtaji wake utaishia hapo hapo, nanyi nimekuja kuwaonya msije kuangukia kwenye kosa la uhujumu uchumi” alisema Mhe. Mtanda.

Mhe Mtanda amesema zoezi la anwani za makazi wilaya ya Arusha linaendelea vizuri ambapo kazi ya kuingiza nyumba 122,000 kwenye mfumo wa NAPA imeshakamilika huku Kazi ya kutengeneza na kusimika nguzo elfu tisa likiendelea ambapo Mkuu huyo wa wilaya ametoa kiasi cha Shilingi milioni Moja na laki tano kutoka kwenye mapato yake binafsi ili kufanikisha zoezi hilo ambalo linatarajiwa kumalizika tarehe 30/04/2022.