Mtihani wa darasa la saba 2019 kuanza kesho…wakuu wa shule waonywa

Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania ( NECTA), Dkt. Charles Msonde
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufanyika kwa mitihani ya
kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 unaotarajiwa kuanza kesho Septemba
11 na kumalizima Septemba 12 mwaka huu.


Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.


BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema vituo nane vilivyofungiwa
mwaka jana baada ya kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la
saba vitaendelea kutumia vituo mbadala vilivyopangiwa hadi baraza hilo
litakapojiridhisha kuendelea kutumia vituo hivyo.


Katika mwaka huu 2019, watahiniwa 947,221 wamesajiliwa kufanya mtihani
wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) unaotarajiwa kuanza kesho (Septemba11
na 12 mwaka huu) huku wakuu wa shule zote nchini wakipewa onyo
kutojihusisha na udanganyifu wa mitihani hiyo.


Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde ameyasema hayo leo
Septemba 10,2019 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa
habari na kusema mwaka jana baraza ilifuta matokeo ya Shule za Msingi
zote za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, Shule za Msingi Hazina,
New Hazina (Kinondoni), Aniny Nndumi, Fountain of Joy (Ubungo),
Alliance, New Alliance na Shule ya Msingi Kisiwani zote za Mwanza Jiji)
na Shule ya Msingi Kondoa integrity (halmashauri mji wa Kondoa) kwa
kufanya udanganyifu.


Amesema shule hizo zilifungiwa kufanyiwa au kusimamia mitahani
zitaendelea kupangiwa vituo mbadala ambavyo vitaendelea kutumiwa na
watahiniwa wanaoanza mtihani leo.


Aidha, Dk. Msonde amevitaja vituo vitakavyotumiwa kwa Mkoa wa Dar es
Salaam, kuwa ni shule ya Hazina na New Hazina itatumia Shule ya Msingi
Oysterbay, Shule ya Fountain of Joy na Aniny Nndumi zitatumia Shule ya
Msingi Mbezi, mkoani Mwanza, Shule ya Kisiwani itatumia Kituo cha Shule
ya Msingi Kakebe, Shule ya Msingi Alliance na New Alliance za
Halmashauri Kondoa Mji mkoani Dodoma kituo kitakuwa Shule ya Msingi
Mahina.


Dk. Msonde amesema kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa 451,235
ambao ni sawa na asilimia 47.64 ni wavulana na watahiniwa 495,986 ambao
no sawa na asilimia 52.36. Waliosajiliwa ni wasichana na kuongeza kuwa
kati ya hao, watahiniwa 902,262 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili
na watahiniwa 44,959 watafanya mtihani kwa lugha ya kiingereza ambayo
wamekuwa wakiitumia kujifunzia ambapo mtihani huo utakuwa na masomo ya
Kiswahili, English Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.


Pia ametaja watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 2,678 kati yao 81 ni
wasioona, 780 wenye uoni hafifu, 628 wenye ulemavu wa kusikia, 325 ni
wenye ulemavu wa akili na 864 ni wenye ulemavu wa viungo,” amesema Dk
Msonde.


Dk. Msinde pia ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa Halmashauri
na Majiji kuhakikisha kuwa taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa
zinazingatiwa kwa kuhakikisha mazingira ya vituo kuwa salama, tulivu na
kuzuia mianya inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu na
wasimamizi wot walioteuliwa wameaswa kufanya kazi kwa umakini na
uadilifu kulingana ja kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa.


“Baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika
kujihusisha au kusababisha udanganyifu wa mitihani kufanyika kwa kujibu
wa sheria na kanuni za utumishi wa umma. Tunaomba wadau kutoa taarifa
katika vyombo husika kila mnapobaini uwepo wa mtu au kikundi cha watu
kujihusisha na udanganyifu wa mitihani wa aina yoyote ile,” amesema Dk
Msonde.


Baraza hilo limewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni
vituo maalum vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia
majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi cha kufanyika mtihani
huo kwani hawatasita kufuta kituo chochote endapo litajiridhisha pasipo
shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani hiyo.


pia wasimamizi, wametakiwa kuhakikisha wanalinda haki za watahiniwa
wenye mahitaji maalum kwa kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu
kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye
uoni hafifu.