Tanzania yapokea faru tisa kutoka afrika kusini

Ndege iliyowabeba Faru kutoka nchini Afrika Kusini ikishusha baadhi ya
mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA, Faru hao
wametolewa na Mfuko wa Grumet (GF) kwenda Serikali ya Tanzania

Na Mwandishi Wetu, KIA

Serikali ya Tanzania imepokea Faru Tisa kutoka Mfuko wa Grumet (GF) nchini Afrika Kusini.

Faru
hao wamepokelewa alfajiri Saa 9 jana katika Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kusafirishwa kwa ndege kuelekea
Ikolongo-Grumet iliyopo Hifadhi ya Serengeti.

Aidha
wakati Faru hao wakiwasili nchini, ilielezwa Faru mmoja alifariki akiwa
Afrika Kusini wakati wa harakati za kuwasafirisha kuja nchini.

Hafla
ya kuwapokea Faru hao ilihudhuriwa na viongozi mbalimabli wa Serikali
wakiwamo Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro Anna Mghwira na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Mrisho Gambo, Makamishna wa Uhifadhi wa Taasisi za TANAPA, TFS,
NCAA na TAWA, Wenyeviti wa Bodi wa mashirika hayo na viongozi wengine.

Akizungumza
wakati wa hafla ya makabidhiano kati ya serikali na Mfuko wa Grumet,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu alisema, serikali
itahakikisha inawalinda wanyama hao kwa gharama yeyote.

“Faru hawa tutawalinda kwa gharama zozote iwe za kisanyansi au kienyeji,” alisema Naibu Waziri Kanyasu.

Kwa
upande Kamishna Uhifadhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA),
Dk. James Wakibara alisema wanyama hao walikuwapo muda mrefu

“Kutoweka
kwao ni kwasababu ya matatizo ya ujangiri, baada ya juhudi kubwa
zinazofanywa na Wizara ya Maliasili hatua inayofuatana sasa ni kuanza
kuwarudisha,” alisema Dk. Wakibara.

Kamishna
Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA Dk. Allan Kijazi alisema
wamefarijika kupata Faru watakaoongeza idadi kwenye mfumo wa Ikolojia ya
Serengeti.

Naye
Kamishna Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk. Fredy
Manongi alisema kwa miaka mingi idadi ya Faru ilikuwa ikishuka Tanzania
kwa hivyo mkakati uliowekwa mwaka huu ni kuongeza idadi ya Faru.

“Tunaamini mkakati wetu utafanikiwa kwa sababu nia ni kuongeza idadi ya Faru nchini,” alisema Dk. Manongi.

Mwisho.
Baadhi ya maboksi yaliyobeba Faru walitolewa na Mfuko wa Grumet.

(GF),
kutoka Afrika Kusini na kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania yakiwa
yanalindwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Professa Adolf Mkenda
kushoto akibadilishana jambo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Grumeti (GF),
Stephen Cunliffe katikati na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori nchini
Dk. Maurus Msuha wakati wa mapokezi ya Faru Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro KIA. Kamishna Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA Dk.Allan Kijazi
akizungumzia ujio wa Faru hao nchini Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA).
Pichani ni Makamishna Uhifadhi kutoka kushoto wa pili ni Dk. James
Wakibara TAWA, akifuatiwa na Kamishna Dos santos Silayo TFS, na Dk.
Allan Kijazi TANAPA wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa
kwanza kushoto Dk. Maurus Msuha, pembeni kulia ni Afisa Mawasiliano wa
TAWA Twaha Twaibu. 


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu akisaini nyaraka
muhimu za makabidhiano ya Faru na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Grumet (GF),
Stephen Cunliffe mara baada ya kupokelewa kwa Faru kutoka nchini
Arusha.