Nape nnauye atinga ikulu kumuomba radhi rais magufuli



Mbunge wa Mtama Nape Nnauye akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mazungumzo
yao pamoja na kusamehewa kosa alilofanya Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu









Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mbunge wa Mtama Nape
Nnauye aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuomba
msamaha Rais Dkt. Magufuli  kufuatia tukio  lililotokea miezi iliyopita.










Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli akifurahia jambo pamoja na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye
aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuomba msamaha mara
baada ya kuzungumza na wanahabari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mbunge wa Mtama Nape
Nnauye mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.



Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Rais
wa Tanzania, John Magufuli amesema amemsamehe mbunge wa Mtama (CCM),
Nape Nnauye huku akielezea namna ambavyo mbunge huyo amekuwa akimuomba
radhi.


Akizungumza Ikulu leo Jumanne Septemba 10, 2019 Rais
Magufuli amesema kwa muda mrefu Nape amekuwa akimuomba msamaha kupitia
ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na kuwatumia baadhi ya wazee wa chama
hicho tawala.


Rais Magufuli amesema Nape alifikia hatua ya kwenda
kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, mjane wa Baba wa Taifa,
Maria Nyerere pamoja na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa
Taifa nchini Tanzania, Apson Mwang’onda


“Alienda kwa mzee
Mangula, amefika mpaka kwa Mzee Apson, Mama Nyerere amehangaika kweli
lakini baadaye ni katika hiyohiyo sisi tumeumbwa kusamehe.”


“Leo
nimemuona asubuhi amekuja hapa baadaye nikaona siwezi nikamzuia, ngoja
niache shughuli zangu nimuone nilikuwa na kikao kingine kikubwa
anachozungumza ninaomba baba unisamehe,” amesema Magufuli.


Kiongozi
mkuu huyo wa nchi amesema, “Na mimi nimeshamsamehe tena kwa dhati
kutoka moyoni mwangu, nimeshamsamehe na nimeshamsamehe kweli. Nape nenda
ukafanye kazi, Mungu akujalie.”


“Unamuona kabisa huyu mtu
anaomba msamaha na leo kaniomba aje anione na saa nyingine wasaidizi
wangu wamekuwa wakipata hizo habari,” amesema Rais Magufuli


Awali,
akizungumza Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM
amesema, “nimekuja kumuona (Magufuli) kama baba yangu, lakini mwenyekiti
wa chama changu, Rais wangu kwa sababu wote mnajua mambo yaliyopita
yalitokea ni mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM mwanaye
niliona ni vizuri nije niongee na baba yangu.”


“Kwa hiyo baada ya
kupata fursa nimekuja nimemuona na mle ambamo nilimkosea kama baba
yangu nimeongea naye na baba amenielewa, ameniambia amenisamehe na
amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo
yatakwenda vizuri.”


Mbunge huyo amesema, “kwa kweli kwa dhati ya
moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea
maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua.”


Ingawa si Nape
wala Rais Magufuli waliozungumza hasa kwa nini wamekutana lakini katika
siku za hivi karibuni kuliibuka sauti za viongozi mbalimbali wakiwamo za
wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na Willium Ngeleja
(Sengerema) wakizungumzia suala la waraka ulioandika na makatibu wakuu
wa CCM waliopita, Yusuf Makamba na Abdurahman Kinana.


Wazee hao
wa CCM waliandika waraka huo kulalamikia mambo mbalimbali kwenda kwa
Katibu wa Baraza la ushauri wa viongozi wa CCM, Pius Msekwa
wakizungumzia mmoja wa wanaharakati ambaye amekuwa akiwachafua bila
hatua kuchukuliwa.


Mpaka sasa bado haijafahamika kama hatua
zimechukuliwa na hivi karibuni, Rais Magufuli alisema January na Ngeleja
walikwenda kumwomba radhi kuhusu sauti hizo alizodai kuwa ni za kwao.