Nchi za afrika zaomba kujifunza posta tanzania

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuingia katika historia baada ya nchi nne za Umoja wa Posta Afrika (PAPU), kuomba kufanya ziara ya kimafunzo nchini juu ya uboreshaji wa huduma za posta.

Akizungumza jana jijini Arusha,wakati wa ufunguzi wa kikao cha wasimamizi na watoa huduma wa sekta ya posta barani Afrika na nje ya mipaka ya  bara hilo, Mkuu wa Shirika la Posta nchini , Macrice Mbodo ametaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Burundi, Kenya, DRC na Zimbabwe.

Amesema mkutano huo unaoendelea katika Jiji la Arusha wajumbe wake wanajadiliana kuona jinsi ya uboreshaji wa huduma za posta na kutatua changamoto wanazokutana nazo.

“Lengo la umoja wa Posta Afrika ni nchi zote kutoa huduma zinazofanana katika bara letu, ndio maana kila nchi inapata uzoefu wa nchi zingine, hata sisi yapo mambo hatuyafahamu wenzetu wametutangulia, lakini nasi tumepiga hatua kubwa kwenye uboreshaji wa miundombinu yetu,”amesema.

Bodo amesema moja ya hatua iliyopigwa na nchi ya Tanzania kwa sasa ni utumiaji wa simu ya kiganjani,  katika uagizaji wa mizigo mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuagiza chochote kwa kutumia teknolojia hiyo, bila usumbufu wala kupoteza muda.

Pia amesema  Shirika la posta kama sekta  haitakufa, hata zaidi ya miaka mia moja, kwa sababu watoa huduma wake wanaendelea kujipanga na kufanya mageuzi  ya kutosha kwenye utoaji wa huduma bora ili kusaidia maendeleo katika Bara la afrika.

Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye  amesema wamekua na mikutano mbalimbali kwa makundi tofauti mkoani Arusha  ya  watoa huduma wa sekta ya posta barani Afrika, ili kubadilishana uzoefu  kwa ajili ya kuboresha zaidi  utoaji huduma.

“Lakini leo tutamalizia na kikao cha Mawaziri wa sekta ya posta kwenye bara letu hili na kumalizia na uzinduzi wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), utakaozinduliwa na Rais Samia Hassan Suluhu Septemba 2 mwaka huu,”alisema.

Alisema  jengo hilo ni bora zaidi mkoani Arusha na ni moja ya kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali, hali hiyo imekua furaha kwa Taifa, kuona ndoto ya muasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere  ya kuomba kujenga makao makuu hayo nchini imetimia.

Waziri Nape aliomba wananchi kujitokeza kuungana na Rais Samia, kwenye uzinduzi huo na kuonyesha ukarimu kwa wageni mbalimbali watakaofika mkoani humo.